Ads

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI ‘SHINYANGA MPYA,MTI KWANZ

Mwambawahabari

 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizindua kampeni ya upandaji miti ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ leo Septemba 23,2017-Picha na Kadama Malunde 
*****
 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro ameanzisha kampeni ya upandaji miti yenye kauli mbiu ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ ili kuboresha mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha jangwa katika wilaya hiyo. 
 
Kampeni hiyo imezinduliwa leo Jumamosi Septemba 23,2017 katika manispaa ya Shinyanga na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack kwa lengo la kuboresha mazingira ya mji wa Shinyanga,maeneo ya taasisi,maeneo ya wazi,maeneo yanayozunguka kaya,kandokando ya barabara na sehemu zingine ambazo hazina miti. 
 
Akizindua kampeni hiyo,Telack alisema kutokana na mvua haba katika mkoa wa Shinyanga, kumekuwepo na mabadiliko ya tabia nchi hali inayosababisha kuwepo na hali ya jangwa. 
 
Telack aliwataka wananchi na wadau wote kuhakikisha wanatunza miti hiyo na kuzuia mifugo kuzurura ovyo mitaani. 

“Tutakuwa wakali,kuanzia sasa ni marufuku kwa mifugo kuzurura mitaani,ikikamatwa kwa kila mfugo faini ni kati ya shilingi 50,000/= na 100,000/=,iwe ng’ombe,mbuzi,kondoo au punda, tukikuta mti umekauka faini ni shilingi 50,000/=”,alieleza mkuu huyo wa mkoa. 
 
Naye Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema uzinduzi wa kampeni hiyo umeanza na barabara 25 za mji wa Shinyanga ambapo jumla ya miti 3000 imepandwa na ofisi zote kata 17 za manispaa ya Shinyanga zitaendelea kutekeleza zoezi hilo. 
Alibainisha kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,sasa wilaya hiyo imekuja na teknolojia rahisi ya kumwagilia miti kwa njia ya matone,teknolojia ambayo inatumia maji kidogo lakini inaweza kumwagilia miti mingi na kwa muda wote.
“Tumekuwa tukipanda miti kila mwaka lakini miti hii ilikumbwa na changamoto nyingi wakati wa usimamizi na kusababisha miti mingi kufa,kwa sasa tumekuja na mpango huu mpya wa kupanda miti itayosimamiwa na wananchi na wadau wote”,alieleza Matiro. 
  Alisema kauli mbiu hiyo ya Upandaji miti ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ ina maana ya kuwaasa watu wote wa Shinyanga kuachana na tabia ya kuharibu miti na hivyo wahifadhi miti. 
 
“Tutatekeleza kampeni hii katika halmashauri zote,kila halmashauri itaanzisha kitalu na kuzalisha miche isiyopungua 25,000,kila kata ipande miti isiyopungua 1000 na iwe na kitalu cha kudumu,ofisi za mitaa na vijiji miti 100,vitongoji miti 50,kila mwananchi miti isiyopungua mitatu na taasisi zote zipande miti”,alifafanua Matiro.
 
Aliongeza kuwa ili kufanikisha kampeni hiyo,taasisi mbalimbali zitachangia mbegu,miche na kupanda miti ili kufikia lengo la kupanda miti isiyopungua milioni 1,500,000 kwa mwaka.

No comments