SERIKALI YAIONGEZEA BAJETI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA NCHINI.
Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali imeiongezea Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora nchini kiasi cha shilingi bilioni 2.6
katika Bajeti yake ya mwaka 2017/2018 kwa kutambua na kuthamini majukumu
yake katika Taifa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB),Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maaluum (CCM), Mhe.
Mwantumu Dau Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuiwezesha Tume
hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe. Mwantumu Haji amesema kuwa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikitengewa fedha kidogo
sana katika bajeti kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo hali
inayosababisha Tume hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji
alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali imetenga bajeti ya
Sh. 6,166,978,000 kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni
sawa na ongezeko la asilimia 42.31 ya bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo
ilikuwa Sh. 3,557,589,200.
Alisema kuwa viwango vya ukomo wa
bajeti kwa mafungu, hutegemea vipaumbele vya Taifa na maoteo ya mapato
katika kipindi husika hivyo ongezeko la ukomo wa bajeti ya Tume hiyo kwa
mwaka 2017/18 linaonesha dhahiri kuwa Serikali inatambua umuhimu wa
Tume hiyo pamoja na majukumu yake.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa
Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani
il kuhakikisha mafungu yote ya kibajeti ikiwemo Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora yanaendelea kupata fedha za kutosha ili
kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Napenda kulitaarifu Bunge lako
Tukufu kwamba, tarehe 01/06/2017 Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mfumo wa ukusanyaji mapato ya
ndani ujulikanao kama ‘Revenue Gateway System’ ikiwa ni moja ya mikakati
ya Serikali kuimarisha ukusanyaji mapato yake yatakayowezesha
upatikanaji wa fedha za kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi”,
alifafanua Dkt. Kijaji.
Post a Comment