SERIKALI YALAANI KITENDO CHA KUUMIZWA KWA WANAHABARI
UMUHIMU WA JAMII KULINDA HAKI NA USALAMA WA WANAHABARI
Dodoma, Jumatatu, April 24, 2017:
Serikali imepokea kwa masikitiko
taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari
katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa
pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda
kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa
na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia
vililengwa katika shambulizi hilo.
Tunachukua fursa hii kulaani
kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria
mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na
nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika
migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.
Kifungu cha 7 (1) (a) cha
Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa
wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo
ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu
wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za
Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.
Tunawatakia nafuu ya haraka
wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika
tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba
wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo
husika vilifanyiekazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali
Post a Comment