MAHAKAMA YA WATOTO SULUHISHO YA KESI ZA WATOTO
Mwuonekano wa jengo la Mahakama ya Watoto iliyopo katika Jiji la Mbeya.
…………..
Na Magreth Kinabo – Mahakama ya Tanzania
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu habari za vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo
hivyo, viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa matamko ambayo yanaitaka
jamii kufahamu haki za mtoto ikiwa ni hatua ya kuwaepusha watoto
wasiathiriwe na tabia hatarishi.
Miongoni mwa viongozi hayo ni
Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Afya,Jinsia na
Maendeleo ya Jamii, Mhe. Ummy Mwalimu akiwemo Naibu wake. Dkt. Hamis
Kingwallah na baadhi ya viongozi wengine mbalimbali.
Serikali kwa kushirikiana na
viongozi wa asasi za kiraia na dini mbalimbali wameungana ili
kuhakikisha watoto hao, wanakua katika maadili mema na kuweza kutimiza
ndoto zao.
Mbali na hilo, kuhakikisha kwamba watu wanaowarubuni watoto wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mahakama ya Tanzania kupitia
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano yaani 2015/16 hadi 2019/20, imejenga
Mahakama nyingine ya watoto ambayo iko katika Jiji la Mbeya.
Kupitia mpango huo, hivi sasa
Tanzania ina mahakama mbili za watoto ambazo moja iko katika jiji la
Dares Salaam na nyingine jiji la Mbeya.
Mahakama hizi mbili ziko katika
maeneo ya katikati ya jiji, ikiwa dhamira ya Mahakama ya Tanzania,
kuhakikisha kwamba inaboresha huduma za utoaji haki na kusongeza
huduma zake karibu na wananchi.
Mahakama ya Watoto ni Mahakama ambayo imeanzishwa kisheria kwa lengo la kushughulikia kesi maalum zinazohusu watoto.
Umri ambao Mahakama hiyo mtoto ni
mtu aliye na umri wa chini ya 18 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 inavyosema sura ya kwanza, kifungu cha 5.-(1) na
ilivyo katika Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni
zake, marekebisho ya mwaka 2006.
Mahakama hii inashughulikia makosa mbalimbali ambayo yanaweza kufanywa na watoto kama shuleni, mitaani na sehemu nyinginezo.
Kuna mambo mbalimbali ambayo
pia Mahakama hii inayashughulikia mfano vile taratibu za kuasili
watoto na mambo ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na mchakato mzima wa
kufanya hivyo, ikiwemo kupokea mashauri ya madai.
Usikilizaji wa mashauri katika
Mahakama hii, hufanyika faragha. Lengo la usikilizaji wa mashauri haya
kusikilizwa kwa siri ni kulinda maslahi ya mtoto.
Hivyo jamii inapaswa kuzifahamu
haki za mtoto kama vile haki ya kuishi, kupata huduma bora za afya,
mahali pa kuishi.kupata elimu, haki ya kutambuliwa, haki ya kurithi
mali, haki ya kutonyanyaswa, ikiwemo kutofanyiwa vitendo vya ukatili
wa kijinsia.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Sihaba Nkinga, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Kuzuia Ukeketaji,iliyofanyika Desemba 5, mwaka jana,
Sihaba Nkinga, alisema hali bado ni mbaya.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba
taarifa zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watatu wa kike na mtoto
mmoja wa kati ya saba wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono.
Kupitia maadhimisho hayo, Mkuu wa
Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, Bi Zainabu Issa ametaka jamii ipige
vita vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ili kuwawezesha kufikia ndoto
zao ikiwa ni hatua ya kuwawezesha ustawi wa maisha yao na hatimaye
kulijenga taifa la kesho.
“Ninasema kesi dhidi ya ukatili wa
watoto sasa zisizidi miezi sita au mwaka, kesi zisikae, muda mrefu
Mahakamani.Ninasema sasa mtu akipatikana na hatia ya kuumpa ujauzito
mwanafunzi au kubaka afungwe miaka 30 jela,” alisema Mkuu huyo wa wilaya
wakati siku ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Mkoani Tanga, wilaya ya
Pangani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Ali Appi akizungumza maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini
Dar es Salaam, alipiga marufuku vitendo vya baadhi ya walimu kuwafungia
mageti wanafunzi wanapochelewa kufika mashuleni kwa kuwa vinaweza
kuwasababishia watoto kujiunga na makundi yenye tabia hatarishi.
Alisema ili kuweza kuwaepusha
watoto kutoathiriwa na tabia hatarishi, Mkuu huyo alipendekeza walimu
watumie adhabu mbadala pale baadhi ya wanafunzi wanapofanya makosa
wakiwa mashuleni.
Alisema adhabu mbadala zinaweza kutolewa na walimu, wakati wa kipindi cha mapunziko.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya
Mwanzo Mjini Mbeya, Mhe. Onesmo Zunda akizungumzia kuhusu uzoefu wa
usikilizaji kesi za watoto zinazohusiana na madai alisema amekuwa
akisikiliza kesi za ndoa na talaka nyingi kutoka vijijini kuliko
mjini.
“Kuna changamoto katika
kusikiliza kesi hizi. Miongoni mwa changamoto tunazokabiliana hizo ni
mgawanyo wa mali hasa pale inapotoa mtu anapokuwa amefariki dunia au
wazazi kutengana mmojawapo akiwa ana fedha au mali au kaoa mke
mwingine. Nyingi hivyo mgawanyo wa mali huwa unaleta malalamiko
katika baadhi ya familia,” alisema Mhe. Zunda.
Alifafanua kwamba katika kesi
hizo ni Baba anapotaka kubaki na watoto halafu mama hataki. Hata hivyo
anasema Mara nyingi mama huwa anataka kubakia na watoto, lakini baba
hataki kutokana na tabia ya mama.
“Hivyo tunatumia sheria pale
ndoa inapotaka kuvunjika tunachoangalia zaidi ni maslahi ya mtoto
hata kama mtoto ana umri wa zaidi ya miaka 7,” anasititiza Mhe.
Zunda.
Akitolea mfano wa kesi mojawapo,
ambapo alisema alitoa maamuzi kwamba mtoto abaki kwa baba kwa
sababu mama alikuwa na tabia ya ulevi. Alisema uamuzi huo kwa
mujibu wa shuhuda za watoto.
Ingawa kulingana na sheria ya
ndoa ya mwaka 1971 ni jukumu la baba kuwapa watoto matunzo japo jukumu
la kuwalea watoto ni la wazazi wote. Hatahivyo, mwanamke anatakiwa
achangie katika kuhudumia watoto. Iwapo wazazi wametengana amri ya
matunzo hutolewa na Mahakama ili baba asiyeishi na mtoto.
Matunzo hayo huwa ni pamoja
na kutoa nguo, chakula, kugharamia masomo shuleni na matunzo
yataendelea hadi kufikia umri wa miaka 18.
“Licha ya changamoto tunazozipitia tunajitahidi kuzitatua kwa kutumia sheria ,hakuna rufaa zinazofunguliwa,”alisema Mhe. Zunda.
Mhe. Zunda alizitaja takwimu za
kesi za ndoa na talaka walizozipokea kwa kipindi cha mwaka huu yaani
Januari hadi Machi 23,mwaka huu, kuwa 26 na hivyo kati ya hizo 11 bado
zinaendelea kushughulikiwa na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa, Mhe. Happiness Chuwa, alisema ili
kukabiliana na tatizo la kesi zinazo husiana na watoto ni vema jamii
ikiwa ina tabia ya kuwatambulisha watoto na kuandika wosia.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Watoto, iliyopo eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es
Salaam, Devotha Kissoka, akizungumza wakati wa Wiki ya Sheria
iliyofanyika mwaka huu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es
Salaam, alisema mtoto akikosa anaweza kupelekwa katika makao ya watoto.
Ikiwa kuna tatizo, ambalo limeleta
mabishano kuhusu mtoto baba yake au wazazi wake ni wakina nani?
Mahakama hiyo inatoa amri Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya vipimo vya
utambuzi (DNA testing).
Alizitaja takwimu zinazohusu kesi
za madai katika Mahakama hiyo za kipindi cha mwaka 2016 ni 154 na
katika kipindi cha mwaka 2015 zilikuwa kesi 19.
Hakimu huyo alifafanua kwamba
sababu ya kuongezeka kwa kesi hizo ni hali ya uchumi, hivyo hali hiyo
imetokea kwa watoto walio nje ya ndoa.
Alisema Mahakama hiyo, pia huwa inasikiliza kesi za jinai mfano wizi wa kutumia silaha, kujeruhi na kuua.
Mhe. Kissoka aliongeza kwamba
ieleweke kwa mujibu wa Sheria, mtoto aliyechini ya umri wa miaka kumi
hawezi kutenda kosa la jinai.
Desemba 5, mwaka huu Tanzania
iliazimisha Maadhimsho ya Kupiga Vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto,
mfano kufanyishwa kazi ngumu, kubaka na kuolewa chini ya umri mdogo, au
kutopewa fursa ya kupata elimu bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Mtoto ana haki ya kupata dhamana katika mashitaka yote isipokuwa yale, ambayo sheria imemtaka hayana dhamana.
Mhe. Kisoka alizitaja adhabu
ambazo hutolewa kwa mtoto, miongoni mwa adhabu hizo ni kuachiwa kwa
masharti kwa kipindi fulani, lakini kisizidi miaka mitatu, adhabu ya
kulipa faini, adhabu ya kuripoti kwa Afisa Ustawi wa Jamii, adhabu
ya kupelekwa katika shule maalum.
Pamoja na adhabu hizo mahakama ina uwezo wa kutoa amri mbalimbali kama vile kulipa faini, kuachiwa bila masharti yoyote.
Kutokana na maoni ya watu
mbalimbali mfumo mmoja wa kisheria na nguvu za pamoja zitasaidia
kupunguza au kutokomeza vitendo vya kikatili na unyanyasaji dhidi ya
watoto.
Hii inatokana na sababu bado umri
wa mtoto bado ni tatizo kwa kuwa mtoto ana weza kuolewa akiwa na
umri wa miaka 14 au kuoa wakati huohuo mtu anaitwa mtoto akiwa na
umri chini ya miaka 18.
Post a Comment