WANAWAKE WATAKIWA KUWASHIRIKISHA WANAUME KUTATUA BAADHI YA CHANGAMOTO.
mwambawahabari
Jovina Bujulu
Mizigo mikubwa waliyonayo wanawake ni miongoni mwa
changamoto za kijamii ambazo zimekuwa kikwazo kwa wao kushiriki kikamilifu
katika masuala ya siasa.
Hayo yamesemwa na Balozi Getrude Mongella ambaye
pia ni Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika alipokuwa akizungumzia ushiriki
wa wanawake katika siasa nchini.
“Changamoto kubwa ni pamoja na teknolojia duni
ambayo inamlazimisha mwanamke kuendelea kulima kwa kutumia jembe la
mkono, kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kutafuta kuni na suala zima
la kulea watoto” alisema Balozi Mongella.
Akizungumzia suala la teknolojia duni alisema kuwa
katika nchi zinazoendelea hilo limeendelea kuwa tatizo kubwa na kwa
kuwa wanawake ndio wazalishaji mali wakubwa, wamejikuta wanaweka nguvu
zao nyingi katika matumizi ya jembe la mkono. Hivyo ukulima kwa kutumia
jembe la mkono haukidhi mahitaji yao ya chakula katika familia na kujikuta
wamebaki kuwa omba omba.
Pamoja na changamoto hizo Balozi Mongella amesema
kuwa ushiriki wa wanawake bado ni mkubwa na ameitaka jamii kuwawezesha
kubeba baadhi ya mizigo kwa mfano kuimarisha huduma za afya ya jamii.
Balozi Mongella alitoa ushauri kwa jamii kutokukaa
kimya bali kuzungumzia changamoto hizo na utatuzi wake ikiwa ni pamoja
na kuwaelimisha wanaume, kwani wakielimika na kutumika vizuri baadhi
ya changamoto zitaondoka na kasi ya mwanamke kupiga hatua itakuwa kubwa.
Aidha, alivitaka vyama vya wanawake kuamka na kuendeleza
mapambano ya kumkomboa mwanamke kwani ajenda ya wanawake ni ya
kudumu na haijakamilika hata kidogo.
Zaidi ya hayo, Balozi Mongella amewataka wanawake
kutambua nafasi yao katika kuchangia uchumi wa taifa, ili wafike mahali
waonyeshe mchango wao katika Tanzania ya viwanda ambayo Watanzania wanaitaka
na kuwashauri wanawake waliopata elimu kusaidia kuwavusha wanawake wengine.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo ambaye
alikuwa Mgombea Urais pekee mwanamke katika uchaguzi uliopita wa 2015,
Mama Anna Mgwira alisema wanawake wakipewa nafasi wanajitoa kwa ukamilifu
hivyo aliwataka wasimamie nafasi zao huku wakifanya kazi kwa weledi,
uaminifu, wajiheshimu na wawajibike ili kuondokana na dhana ya kwamba
hawawezi kazi bila kusimamiwa na kusaidiwa.
Post a Comment