UELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI, WADAU WATAKIWA KUONGEZA FURSA ZA UCHUMI KWA WANAWAKE.
Jovina Bujulu
mwambawahabari
Kila mwaka ifikapo Machi 8 kila mwaka, wanawake duniani
kote huadhimisha siku yao ambapo hujitathmini kupitia shughuli
mbalimbali za maendeleo walizofanya, changamoto zilizopo na kuweka mikakati
ya utatuzi wa changamoto hizo.
Akiongea hivi karibuni katika kuelekea maadhimisho
ya siku ya wanawake duniani, Katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Maendeleo
ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Sihaba Nkinga alisema kuwa kauli
mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya Viwanda; Wanawake
ni Msingi wa Mabadiliko”
Kauli mbiu hii inasisitiza kuwajengea wanawake uwezo
wa kitaaluma, kibiashara, upatikanaji wa mitaji, masoko na biashara
ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika na fursa zilizopo badala
ya kuwa wasindikizaji.
“Ujumbe wa kauli mbiu hii umezingatia sera ya maendeleo
ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 na ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu
hususani lengo namba 5 kuhusu usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake
kiuchumi” alisema Bi Nkinga.
Kauli mbiu ya mwaka huu imetotolewa kutokana na kauli
mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN) isemayo “Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi
katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi wa Chama cha
Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) Mama Edda Sanga alisema kuwa wanawake
wanapaswa kujiwezesha katika maeneo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii
ili wapate fursa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ambayo hatimaye
yatawaletea tija na mafanikio.
Hii ina maana kuwa, endapo wanawake watapata nafasi
ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ni rahisi kwao kusikilizwa na
hata kuwa na sauti katika masuala ya wao kumiliki ardhi, majumba na
hata viwanda.
Aidha, kauli mbiu hii inawahamasisha wanawake kuhakikisha
kuwa kunakuwa na usawa wa jinsia unaoondoa vikwazo na kuhakikisha wanapata
fursa sawa na kuweka ulinganifu katika ushiriki ambao unawanufaisha
kiuchumi kuanzia ngazi ya familia.
Ili kufikia malengo ya kujikomboa kiuchumi, wanawake
wanatakiwa kujitambua na pia kutambua malengo na mipango yao. Wanatakiwa
kutambua na kutumia fursa vizuri wanayopata hasa mahali watakapopata
taarifa za kuwanufaisha kiuchumi kwa mfano benki, vikundi vya mikopo,
taasisi au hata kwa watu binafsi.
Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwakwamua wanawake
kiuchumi, kutoka kwenye taasisi, mashirika na watu binafsi, hata
hivyo wao pia wanahitaji kujikomboa kwa kutumia juhudi zao binafsi kama
vile kujiunga katika vikundi waweze kukopeshwa ili waweze kujiajiri
katika mkondo wa uzalishaji mali, kama vile kuanzisha viwanda vidogo
vidogo, kwa mfano viwanda vya usindikaji vyakula, kazi za mikono na
ushonaji ambavyo havihitaji mtaji mkubwa.
Hii itawafanya kunufaika na kuondoa hali ya utegemezi
katika jamii, na hivyo kujiondoa katika hali ya unyonge.
Ni ndhahiri wanawake ndio wazalishaji wakubwa katika
nyanja za kiuchumi, hivyo katika kutimiza ndoto na malengo zao ni budi
juhudi zitumike ili washiriki katika kukuza pato lao na taifa kwa ujumla.
Naye Bibi Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao
wa Jinsia Tanzania (TGNP) anasema kuwa katika kusherekea siku ya wanawake
duniani, taasisi yao ilifanya kongamano hivi karibuni pamoja
na mambo mengine walizungumzia mpango wa taifa kuhusu ushiriki wa wanawake
katika kuelekea uchumi wa viwanda vya kati.
Alisema kuwa wanawake wa mjini kwa sasa wanashiriki
vizuri katika shughuli ambazo huwaongezea kipato wakati wanawake
wa vijijini ushiriki wao katika shughuli za kuwaongezea kipato si wa
kuridhisha kwani wanatumia muda mrefu kutembea kutafuta maji na kuni
kwa ajili ya matumizi ya familia.
Bibi Liundi alitoa wito kuwa huduma za jamii zisogezwe
karibu na jamii ili wanawake ambao ni wazalishaji mali wakubwa wapate
muda wa kutosha kushiriki katika shughuli za kujiongezea kipato badala
ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Naye Bibi Magreth Dotto ambaye ni Mhandisi wa Migodi,
na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam aliwashauri
watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa kuzingatia kasi ya ukuaji
wa teknolojia kila siku ili baadaye wapate nafasi nzuri katika jamii
na kutoa mchango wao katika kutatua changamoto za kijamii na taifa.
“Uhandisi unawezekana kwa wasichana na ni taaluma
nzuri, hivyo wasichana waache kuyaogopa masomo ya sayansi, ni taaluma
inayobadilisha maisha kwa kuyaboresha kwa sababu inalipa vizuri” alisema
Bibi Magreth.
Kwa upande wake Dkt. Ave Maria Samakafu ambaye ni
Mhadhiri katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Mratibu wa Taifa
wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo alisema kwa sasa wanawake wana mwamko
mkubwa ambao umeleta mageuzi katika familia na kuinua kipato chao.
“Kwa sasa tunaona ushiriki mkubwa wa wanawake katika
nyanja ya uchumi kwa sababu kuna wanawake wafanyabiashara wadogowadogo,
wa kati na hata wakubwa” anasema Dkt Semakafu.
Alisema kuwa elimu inahitajika zaidi kwa wanawake
wa vijijini ambao bado wanatawaliwa na tafsiri potofu ambapo ukandamizaji
wa wanawake bado unapewa nafasi kubwa na jamii, hivyo kuwafanya wasisonge
mbele katika kujiletea maendeleo yao.
Dkt. Semakafu aliendelea kusema kuwa wanawake wengi
wa mjini wanatambua nafasi zao katika jamii, hivyo wanatumia ufahamu
huo kama fursa kwao ambazo zinawasaidia katika kuleta mageuzi ndani
ya familia zao.
“Vijana wa kike wamekuja na nguvu mpya, kinachoendelea
sasa hivi kinafungua uelewa wa jamii, watoto na wazazi na kuwafanya
watambuliwe na jamii” alisema Dkt. Semakafu.
Dkt. Semakafu alitoa mfano unaodhihirisha nafasi
ya mwanamke akimtaja Agnes Magongo ambaye hivi karibuni ameshinda tuzo
ya UN ya “women economic empowerment” ambayo ni tuzo ya uwezeshaji
wa wanawake.
“Wanawake tushiriki katika kuboresha maisha yetu,
tusiwe wasindikizaji bali watendaji, twende pamoja katika uchumi wa
viwanda ili tuweze kumiliki viwanda” alimalizia Dkt. Semakafu.
Katika kuhimiza fursa za uchumi kwa wanawake kauli
mbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote nchini kuongeza
fursa za kiuchumi kwa wanawake ili waweze kushiriki na kunufaika nazo
hasa kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea azma ya uchumi wa kati kwa
misingi ya kuwa nchi ya viwanda.
Mama Sihaba aliwakumbusha wadau wote katika ngazi
zote kuweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto zinazokwamisha kufikiwa
kwa usawa wa jinsia na kusababisha wanawake na wasichana kushindwa kutimiza
malengo na ndoto zao kimaisha.
Post a Comment