WAAJIRI WATAKIWA KUWASILISHA MICHANGO YA FIDIA KWA WAFANYA KAZI KWA WAKATI NA KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI
Na Maria Kaira
mwambawahabari
Serikali imewataka Waajiri wote nchini kuwasilisha michango yao kwa wakati pamoja na kuboresha mazingira ya kazi ikiwa na lengo la kuwawezesha watumishi wao kupata huduma bora za kimatibabu pindi waumiapo au kuugua wawapo katika maeneo yao ya kazi.
Agizo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Ulemavu Jenista Mhagama wakati akizindua huduma za utoaji wa mafao ya fidia kwa wafanyakazi na ubia kati ya mfuko na watoa huduma za Afya.
Pia Mhagama amesema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo kwa wafanyakazi hapa nchini ni kuwasaidia na kutatua kilio chao cha muda mrefu kwa wafanyakazi walio kwenye sekta za umma na binafsi, ambao walikuwa wakilalamikia huduma zinazotolewa sio za kulidhisha pindi wanapopata matatizo wawapo makazini.
"Lazima jitihada ziongezeke kwa kutoa elimu na kuboresha huduma ili ziweze kuwafikia watanzania wote, uchangiaji wa mafao sio ya hiari ila nilakisheria kwa kila mwaajiri kuhakikisha anawasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati,sisi serikali kwa kulitambua hilo kwa mwaka huu wa fedha tumeshawakilisha michango yetu kwa wakati"amesema
Aidha waziri Mhagama ametoa wito kwa Bodi ya mfuko huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria zilizopo, pia wahakikishe wanakuwa na watoa huduma waaminifu ili kuondoa uwezekano wa mfuko huo kuingia gharama zisizokuwa halisi na kujikuta wakighalamia matibabu ambayo hayatokani na ajali, magonjwa yatokanayo kazini.
Hata hivyo waziri Mhagama ameutaka mfuko huo kujitangaza zaidi kwa kukutana na wawakilishi wa waajiri na wafanyakazi kwa lengo la kujadiliana majukumu yao pamoja na matarajio yao ya baadae.
“Ni lazima tutambue wanaotufanyia kazi ni Binadamu na hakuna binadamu aijuaye kesho yake hivyo changieni mfuko huu kwa moyo mmoja sio tu kwa sababu ni kisheria bali kama motisha kwa wafanyakazi kila mwajiri awajibike kumchangia mfanyakazi wake"
Pamoja na hayo Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko WCF, Masha Musomba amesema wamekuwa wakikutana na Changamoto mbalimbali ikiwa pamoja nakutopata taarifa sahihi za nyuma za watumishi waliopata ajali wakiwa kazi pamoja na uelewa Mdogo kwa watanzania.
"Hata hivyo mfuko wetu umeweza kuingia ubia na taasisi saba za utoaji huduma za afya hapa nchini, ikiwa pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Emmanuel Homba amesema kupitia mfuko huo utaweza kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi pamoja na kulinda Afya za wafanyakazi wawapo kazini.
Post a Comment