Tanzania Kufungua Ofisi za Ubalozi Nchini Jamhuri ya Korea
Na: Frank Shija
mwambawahabari
Tanzania yadhamiria kuimarisha uhusiano baina yake na Jamhuri ya Korea kwa kufungua Ofisi zake za Ubalozi Mjini Seoul, nchini Korea.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea msaada wa Dola za Kimarekani 50,000 kwa ajili ya kusaidia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika kutokana na Tetemeko la Ardhi lilitokea Mkoani Kagera mnamo tarehe 9 Septemba 2016.
Balozi Mahiga amesema kuwa nchi ya Jamhuri ya Korea imekuwa na uhusiano mzuri na wa muda mrefu na Tanzania ambapo kupitia uhusiano huo imekuwa ikisaidia katika mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya akitolea mfano Hospitali za Mloganzila na Chanika ambazo zote zimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Mahusiano la Korea (KOICA).
“Korea imekuwa na Ofisi za Ubalozi hapa nchini kwa zaidi ya miaka 25 hivyo wameona ni wakati sasa kwa Tanzania kuwa na Ofisi yake Ubalozi nchini nnchini Korea,” Alisema Balozi Mahiga.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Bw. Song, Geum – Young amesema kuwa msaada huo unatokana na namna ambavyo waliguswa na janga la Tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na makazi ya wananchi.
Ameongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa Rais Dkt. Magufuli alipomtembelea Ikulu na kumpa Pole mnamo tarehe 22 Septemba mwaka huu.
Balozi Song Geum-Young pia amemhakikishia Waziri Mahiga kuwa Korea itaendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kwamba itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa Daraja la Salender, Meli, Hospitali ya Mloganzila, Chanika na mingineyo.
Post a Comment