NIMR NA WIZARA YA AFYA WATOFAUTIANA KUHUSU KUGUNDULIKA VIRUSI VYA ZIKA NCHINI
Na Maria Kaira
mwambawahabari
Kufuatia na taarifa zilizothibitiswa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuhusu kugunduliwa kwa Virusi vya Zika nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu ameibuka na kusema wizara yake hadi sasa bado haijapokea taarifa yoyote kutoka NIMR kuhusu ugonjwa huo zaidi ya kuzisikia taarifa hizo kwenye vyombo vya habari jana usiku na leo.
Pamoja na hayo waziri huyo amesema ugonjwa wa ZIKA unatolewa taarifa kimataifa na kuongeza kuwa tayari amemuita Mkurugenzi Mkuu wa NIMR ili afike ofisini kwake na atoe ufafanuzi kuhusu taarifa yake aliyoitoa kisha wizara itatoa taarifa rasmi kwa wananchi leo mchana.”
Katika taarifa aliyoiandika kwenye akaunti yake ya Facebook, Waziri Ummy amesema:
“Hadi sasa Wizara ya Afya haijapokea taarifa yoyote kutoka NIMR zaidi ya kuzisikia ktk vyombo vya habari jana usiku na leo. Lakini nisisitize kuwa ZIKA ni ugonjwa unaotolewa Taarifa kimataifa (International reportable disease).
Tuna International Health Regulations (IHR) Focal Point ambayo ndiyo ana mamlaka ya kutangaza mlipuko wa ugonjwa huu na magonjwa mengine kama haya baada ya kushauriana na Mganga Mkuu wa Serikali (CMO) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Nimemuita Mkurugenzi Mkuu wa NIMR afike ofisini kwangu asubuhi hii ili atoe ufafanuzi kuhusu taarifa yake aliyoitoa. Tutatoa taarifa rasmi kwa wananchi leo mchana.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya NIMR, Dkt Mwele Malecela, virusi hivyo vimepatikana katika mikoa miwili ya Tanzania, Morogoro na Geita na utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.
“Bado tunajaribu kuangalia ni aina gani ya virusi vya ZIKA. Lakini hiyo ni dhahiri, tukizingatia kwamba mbu wanaoambukiza ugonjwa wa ZIKA wako nchini kwetu na mazingira yaliyoko nchini kwetu hayatofautiani sana na yale ya Amerika ya Kusini na nchi kama Thailand ambako ugonjwa huo unapatikana,” amesema Malecela.
Virusi vya Zika zimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo katika mataifa ya Amerika Kusini na hasa Brazil.
Post a Comment