MPANGO BORA WA MATUMIZI YA ARDHI KUNUFAISHA VIJIJI 30
Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari
Mpango Bora wa Matumizi ya Ardhi utakaobainisha mipaka kati ya Kijiji kimoja na kingine pamoja na maeneo husika ya makazi unatarajiwa kunufaisha jumla ya Vijiji 30 nchini.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Meneja Miradi wa Shirika la PELUM – Tanzania, Rehema Fidelis wakati wa mafunzo kwa wajumbe wa Halmashauri za Vijiji, Mabaraza ya Ardhi, Kamati za Maamuzi pamoja na wananchi yaliyolenga kuwaongezea maarifa na uelewa ili kuimarisha haki za ardhi kwa wakulima wadogo chini ya Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Sekta ya Kilimo.
Bi. Rehema alisema kuwa shirika hilo limeamua kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyokithiri nchini inapata suluhisho kwani wamebaini kuwa vijiji vingi havijafanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi jambo linalochochea kuwepo kwa kutokuelewana baina ya kijiji kimoja na kingine na hivyo kuibua migogoro ya ardhi.
“Vijiji vitakavyonufaika ni vya Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Iringa ambapo mpango huu utasaidia kubainisha maeneo ya shughuli za kijamii, malisho na kilimo kama njia mojawapo ya kupunguza migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji na wawekezaji,” alisema Bi. Rehema.
Amefafanua kuwa mpango huo unatarajia kunufaisha wananchi 10,000 toka vijiji 30 vya wilaya za Morogoro mjini na Mvomero, Bahi na Kongwa (Dodoma) pamoja na Kilolo na Mufindi (Iringa) ambapo kila wilaya itawakilishwa na vijiji vitano.
Akibainisha matokea ya awali ya mradi huo, Afisa Mipango Miji wa Wilaya ya Kongwa, Meshack Sylvester alisema kuwa mafunzo waliyopewa wanakijiji hao yamewafanya kuwa na uelewa hivyo kukubali kukaa pamoja na uongozi wa vijiji vyao kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya amani.
Mbali na kufanikiwa kutatua migogoro hiyo, Sylvester alisema kwa sasa jamii imekuwa na uelewa juu wa wanawake kuweza kupata fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa ardhi kama ilivyo kwa wanaume.
“Awali wanawake walikuwa wakinyanyasika kutokana na mila na desturi, hivyo kukosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kumiliki, kuuza na kurithi ardhi lakini kwa sasa jamii imepata uelewa na wapo wanawake ambao tayari majina yao yameingizwa kwenye idadi ya watu ambao watapata hatimiliki za kimila za mashamba yao wakati zoezi likiendelea” alisema Sylvester.
Ameongeza mafanikio mengine ya mradi huo kuwa ni kuweza kuundwa kwa kamati 26 za kushughulikia migogoro midogomidogo ya mipaka na haki za wanawake walemavu na wajane kwani mwanzo kabla ya mradi kulikuwa na kamati tano pekee.
Naye mkulima kutoka kijiji cha Lenjulu wilayani Kongwa, Yohana Sulutya amelipongeza zoezi hilo kwani litatatua migogoro ya ardhi katika vijiji vyao pia mafunzo waliyopatiwa yamewasaidia kufahamu sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi ikiwemo kujua kuwa wanakijiji ndio wenye mamlaka ya mwisho juu ya ardhi ya kijiji pamoja na kufahamu kuwa viongozi wa kijiji na kamati husika za masuala ya ardhi hawana mamlaka ya kuuza ardhi ya kijiji pasipo maridhiano na wanakijiji kupitia mkutano mkuu wa kijiji.
Naye Samwel Saning’o mfugaji kutoka Kijiji cha Kibaoni wilayani Mvomero, alikiri kuwepo kwa migogoro ya ardhi mara kwa mara katika wilaya ya Mvomero baina ya wakulima na wafugaji, na kubainisha kuwa migogoro mingi inachangiwa na wanavijiji kutokufahamu mipaka ya vijiji yao ikiwa ni pamoja na vijiji kutokufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuchangia kufuata malisho, majosho ama maji ya mifugo maeneo ya mbali.
Kwa upande wake Fransisca Mtizi kutoka kijiji cha Kongogo Wilaya ya Bahi aliiomba Serikali kumalizia kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vilivyobaki pamoja na kugawa hatimiliki za kimila kwenye mashamba ya wakulima wengine ambao vijiji vyao havikuingia kwenye mradi huu ili kuleta usawa baina yao.
Post a Comment