Serikali ya Kuwait yaahidi kuisaidia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) vifaa tiba
Serikali ya Kuwait imeahidi kuisaidia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) vifaa vitakavyotumika katika utunzaji na utoaji wa damu , mashine na vifaa vya upasuaji ambavyo vitatumika katika chumba cha upasuaji.
Ahadi hiyo imetolewa leo na Balozi wa nchi hiyo Mhe. Jasem Al Najem alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuangalia ni jinsi gani nchi yake inaweza kuisaidia katika upatikanaji wa vifaa tiba.
Mhe. Balozi Al Najem alisema vifaa vitakavyotumika katika utunzaji na utoaji wa damu vitapatikana kabla ya kumalizika kwa mwaka huu ambapo vifaa pamoja na mashine za upasuaji vitapatikana mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2017.
“Serikali ya nchi yangu inaangalia namna ya kushirikiana zaidi na Taasisi hii pamoja na Taasisi zingine zilizopo Dar es Salaam, Zanzibar na maeneo mengine hapa nchini ili watanzania waweze kupata huduma bora”, alisema Mhe. Balozi Al Najem.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuahidi kuwapatia vifaa pamoja na mashine zitakazotumika katika matibabu ya wagonjwa wa moyo.
“Tuna vyumba vitatu vya upasuaji, vinavyotumika ni viwili kwani kimoja hakina vifaa, kupatikana kwa vifaa pamoja na mashine kutoka nchini Kuwait kutatufanya tuwe na vyumba vya upasuaji vitatu ambavyo vitasaidia kutoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa .
Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Al Najem alitembelea vyumba vya upasuaji wa moyo, chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) na kutoa zawadi kwa watoto waliolazwa.

Post a Comment