Ads

RAIS WA SHIRIKISHO LA FILAMU AIOMBA SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA FILAMU NCHINI.




Na. Lorietha Laurence-Mwanza
Mwambawahabari
Rais wa Shirikisho la Filamu Nchini Bw.Saimon Mwakifwamba ameiomba Serikali kupitia Bodi ya Filamu nchini kuendeleza  ushirikiano wa kutoa warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa tasnia hiyo  kwa ngazi zote za  Mkoa na Wilaya ili kuwafikia wadau wengi zaidi.

Bw.Mwakifwamba aliyasema hayo  Jijini Mwanza katika warsha ya kuwajengea uwezo wanatasnia wa filamu iliyoandaliwa na Bodi ya Filamu nchini kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF kanda ya Ziwa yenye  lengo la kuboresha sekta hiyo na kuwa chanzo kikuu cha uchumi binafsi na wa nchi.

Aidha anaongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo wanatasnia wameweza kujifunza fursa mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii katika kuboresha maisha yao ya kazi na familia na jinsi ya kujipatia masoko kupitia mitandao ya kijamii.


“Tunaishukukuru Serikali kupitia bodi ya filamu nchini  kwa fursa hii ambayo imetufungua macho ya kuona mbali zaidi  ikiwemo uwekezaji kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii na umuhumi wa taaluma na weledi katika kuandaa filamu bora alisema Mwakifwamba.

Aliongeza kuwa filamu ni biashara na ajira iliyo na manufaa kwa nchi na wananchi wake  hivyo ni wajibu wa wanastnia hao kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa ili kuweza kufika mbali zaidi  na kuteka soko la Kimataifa.

Pia aliwataka wanatasnia hao kuwa na umoja na mshikamano kwa kuwa hiyo ndiyo nguzo pekee ya kuwawezesha  kufanikiwa na kuendelea  katika kufanyia  kazi taaluma na vipaji vyao.

Naye Afisa Uendeshaji na Masoko wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF Kanda ya Ziwa Bw. Khatibu Musa  amewataka wanatasnia hao kutumia fursa  ya kujiunga na Wote Scheme ili kunufaika na  huduma  za mikopo na bima  ya afya.

Jumla ya wasanii 300, kutoka mkoa wa Mwanza, pamoja na viongozi wa wasanii wa mikoa  ya Geita, Shinyanga na Simiyu wamepatiwa mafunzo ya siku tatu kwa ajili kuwajengea uwezo katika hatua mbali mbali za kuboresha kazi zao za filamu hapa nchini.

No comments