Ads

rais magufuli awaongoza mamia ya watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Spika Mstaafu Marehemu Samweli Sitta



Frank  Mvungi 
Mwambawahabari
RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaongoza mamia ya Watanzania ikiwemo Viongozi wa Chama na Serikali kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Spika Mstaafu Marehemu Samweli Sitta katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisilisha Salamu za Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali imempoteza Kiongozi mwadilifu, mzalendo na mchapa kazi ambaye wakati wote alifanya kazi kwa maslahi ya nchi yake.

Aidha amesema  Taifa limempoteza mtu mnyenyekevu, mwanamapinduzi na mpenda haki aliyejitoa kuwatumikia watanzania kwa takribani miaka 49 ya utumishi wake Serikalini.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi Ferdnand Wambali amesema kuwa Taifa limempoteza mtu Jasiri aliyetetea wanyonge wakati wote na kuishi maisha ya uadilifu.


“Marehemu Sitta aliwahi kuitwa na mahakama ili kutoa ushahidi kwenye kesi ya ajali za barabarani na aliwahi mahakamani siku husika hata kabla ya shughuli za mahakama kuanza saa moja asubuhi yeye alikuwa ameshafika hii ilionyesha unyenyekevu wake” Alisisitiza Jaji Kiongozi  Wambali.

Jaji Kiongozi Wambali ameongeza kuwa wakati wote Marehemu Mhe. Sitta alijitoa kutoa ushauri kila alipohitajika bila kusita na kusimamia kile anachokiamini.

Kwa Upande wake Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mchungaji Chediel Luiza amesema Mhe. Marehemu Sitta alikuwa Kiongozi na mtumishi wa watu katika kipindi chote cha uhai wake.

Aliwataka watu wote kuwatumikia watu wasio na uwezo na uadilifu na upendo ili kutimiza yale yawapasayo kufanya kama Mwenyezi Mungu anavyoelekeza kwa ustawi wa Taifa letu.
Spika mstaafu Samweli Sitta ameshika nyadhifa mbalimbali Serikalini zikiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Uwaziri, Mkuu wa Mkoa,Mkurugenzi wa Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC).

No comments