TFDA YAKAMATA DAWA BANDIA MIKOA YA KANDA YA ZIWA NA NYANDA ZA JUU KUSINI.
mwambawahabari
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo akionyesha baadhi ya dawa bandia zilizokamatwa baada ya ukaguzi maalum uliofanyika maeneo ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini wakati alipoongea na waandishi wa habari katika mkutano wa kutoa matokeo ya ukaguzi wa dawa bandia huo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo katika akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa dawa na bidhaa Nyongeza Bw. Adonis Bitegeko kulia na Msajili wa Baraza la famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe kushoto wakionyesha baadhi ya dawa bandia wakati wa mkutano wa kutoa matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa bandia uliofanyika jijini Dar es salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo hayupo pichani wakati wa mkutano wa kutoa matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa bandia uliofanyika jijini Dar es salaam. (picha na James Ndege)
Mwambawahabari
Na:Rayusa Yasini na John Luhende
Dawa bandia zisizo faa kwa matumizi ya binadamu zimekamatwa katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya ukaguzi maalum wa kutafuta dawa bandia uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa katika maeneo hayo .
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati akitoa Matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa uliofanyika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
“Kutokana na ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda hizo kutafuta dawa bandia na zisizo sahihi kwa matumizi ya binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia aina tano ambazo zipo kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua vijasumu(Antibiotics)” alisema Bw. Sillo.
Aidha Bw. Sillo amesema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata dawa ya malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa katika kiwanda cha Elys Chemical nchini Kenya na nyingine zinatengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.
Mbali na hayo Bw. Sillo amesema kuwa pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi hilo lilifanikiwa kubaini na kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi , zisizosajiliwa zenye ubora duni zenye thamani ya Tsh. Milioni 17.463.
Bw. Sillo ameongeza kuwa Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali ambazo zilionyesha uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara mwezi Agosti na Septemba mwaka huu na kusistiza kwamba zoezi hilo la ukaguzi linaendelea nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza la famasia Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema kuwa wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi.
“Wataalamu wa dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.
Pamoja na hayo amesema kuwa ukaguzi huo ulianza Oktoba 4 mwaka huu na unafanywa kwa ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi na Maafisa kutoka Baraza la Famasia Tanzania na litakuwa endelevu ili kuhakikisha tatizo la dawa bandia linatokomezwa kabisa.
Post a Comment