Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki watekeleza agizo la Rais la Mchango wa Madawati
Na Beatrice Lyimo
Watumishi wa Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wamechangia kiasi cha Tsh.
Milioni 100 ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha umma kuhusu zoezi la upatikanaji wa madawati
katika shule za msingi na Sekondari nchini.
Akikabidhi mchango
huo kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya watumishi wa wizara hiyo,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa watumishi hao
wametoa fedha hizo kwa shule ya msingi Chamazi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la
Rais la upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari nchini.
Balozi Mahiga amesema
Wizara yake iliwahamasisha watumishi wake walio makao makuu na wale walio
kwenye balozi mbalimbali nje ya nchi kuchangia zoezi hilo la upatikanaji wa
madawati.
“Ili kufanisha
upatikanaji wa fedha hizi Wizara yangu iliwahamasisha watumishi wake wote walio
Makao makuu na wale walio katika balozi zetu duniani kote, wito huu uliitikiwa kwa ari na hamasa kubwa na
kufanikisha kukusanya kiasi cha Shilingi 100,176,825.52 za kitanzania”alisisitiza
Balozi Mahiga.
Waziri Mahiga
aliongeza kuwa mara baada ya kukusanya fedha hizo watumishi wa Wizara hiyo waliamua
kumpatia aliyekuwa Mtumishi wa Wizara ambaye sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa
Wilaya ya Manyoni kiasi cha shilingi Milioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa
madawati katika Wilaya yake.
Aidha, amesema kiasi
fedha zilizobaki zaidi ya shilingi milioni 85 zilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa kwa ajili
ya mchango wa utengenezaji wa madawati ya shule ya Msingi Chamazi iliyoko
Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mahiga
aliongeza kuwa mbali na wizara yake kuwa na majukumu mbalimbali bado inalo
jukumu la kuhakikisha inaitangaza Tanzania ili kuvutia wawekezaji na kukuza
uchumi wa nchi, na kuongeza kuwa elimu bora ni msingi imara katika kufanikisha
hilo.
Post a Comment