Naibu waziri Habari afungua mashindano ya Brazuka Kibenki
Na Lorietha Laurence
Serikali kupitia sera ya Maendeleo ya Michezo inasisitiza wananchi na jamii kwa ujumla kushiriki katika michezo ili kujenga afya, kuunganisha watu toka makundi mbalimbali bila ubaguzi wa kidini, kisiasa, wala kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kibenki maarufu kama Brazuka katika viwanja vya Gymkhana leo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Wambura ameeleza kuwa ni muhimu kwa wafanyakazi kujumuika kwa pamoja katika michezo ili kuboresha afya na kuimarisha uhusiano baina yao.
“Michezo ni kitu kizuri kwani husaidia katika kuimarisha na kulinda afya zetu hivyo ni vyema kila mmoja wetu kushiriki katika michezo ili kuwa nguvu ya kutekeleza majukumu yetu ya kila siku” alisema Mhe. Wambura.
Vilevile alitoa shukrani kwa wakuu wote wa mabenki kwa ushirikiano wao wa kuwaleta pamoja wafanyakazi wa benki ili kufahamiana na kuimarisha ushirikiano baina yao .
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Benki ya Barclays Bw. Aron Luhanga amesema kuwa dhumuni la mashindano hayo ni kuendeleza mahusiano baina ya benki kwa kufahamiana na kuimarisha afya na fikra zao.
mashindano haya ni kwa ajili ya kufahamiana na kuimarisha urafiki kwa wafanyakazi wa sekta ya benki kwa kufanya sekta ya kibenki kuwa sehemu bora ya shughuli za kiuchumi nchini alisema Bw.Luhanga.
Mashindano hayo ya Brazuka kibenki yanaratibiwa na benki ya Barclays na ni mara ya pili kufanyika nchini ambapo mwaka jana benki ya Diamond Trust (DTB) iliibuka mshindi hivyo kushiriki katika ufunguzi wa michuano hiyo mwaka huu.
Benki zinazoshiriki mashindano hayo ni 18 ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, NMB, Stanbic, KCB, Exim, Citi Benki, Commrcial Bank of Africa (BOA),CRDB, Letshego, Eco Bwnki, Akiba, Diamond Trust Benki, Bank of India, Banc ABC,Azania na Twiga Bancorp.
Post a Comment