Juhudi za Serikali katika kupunguza umasikini nchini
Na Beatrice Lyimo
mwabawahabariblog
Pamoja na uchumi wa Tanzania kuelezwa kukua kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka katika miaka ya hivi karibuni, hali ya uchumi kwa wananchi nchini imekuwa si ya kuridhisha hasa kutoka na wengi kukabiliwa na umasikini wa kipato uliochangiwa na sababu mbalimbali.
Kihistoria wakati wa ukoloni wananchi waliwekewa vikwazo kushiriki katika uchumi ili watawalike kirahisi wakilazimika kujishughulisha na uchumi wa sekta isiyo rasmi wakati sehemu kubwa ya sekta rasmi ilishikwa na watawala.
Wakoloni walitumia mbinu mahsusi kuwaendeleza wazungu na wananchi wachache ikiwa ni pamoja na utoaji wa mikopo, utoaji wa elimu, ugawaji wa ardhi na utoaji wa leseni za biashara.
Kutokana na hali hiyo Serikali ya Tanzania pamoja na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakipambana kila kukicha ili kijikwamua kutoka katika umasikini wa kukosa hata milo mitatu kwa siku na mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwemo afya, maji, malazi, mavazi na elimu.
Juhudi za kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupambana na umasikini zimekuwa zikitekelezwa kwa mikakati na mipango mbalimbali kuanzia mikakati ya kisekta na mikakati ya mwananchi mmoja mmoja.
Katika kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uchumi, wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ujuzi na uzoefu vikichochewa na upungufu wa elimu, mafunzo, mila na desturi potofu na mtazamo wa kimaendeleo.
Pia ukosefu wa masoko ya uhakika au uwezo wa kuingia katika masoko yenye ushindani, ukosefu wa ushirikiano, ushiriki hafifu na ukosefu wa sauti ya pamoja ya makundi mbalimbali ya wananchi katika kusimamia maslahi yao ya kukubaliana na matatizo yanayowakwaza wasishiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi katika sekta zao.
Awali Tanzania iliamua kupitisha na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) wenye misingi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia inayozingatia matokeo ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kukabiliana na changamoto za kukuza uchumi na kupambana na umaskini nchini.
Mkakati huo unaonesha kuwa kiwango cha umaskini wa kipato kwa wananchi hakikubadilika kwa kiwango cha kuridhisha ambapo kila Watanzania 100, ni Watanzania 36 walikuwa na umasikini wa kipato kwa mwaka 2000/1 wakati Watanzania 34 walikuwa masikini katika kipindi cha mwaka 2007.
Kiwango hiki cha umasikini wa kipato kimetofautiana kutoka eneo moja hadi lingine, maeneo ya vijijini yakiwa na asilimia 38 ya umasikini wa vipato katika mwaka 2007 ikilinganishwa na asilimia 39 ya mwaka 2000/1.
Baadae Serikali ya awamu ya nne ikiongozwa na Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ilipambana vilivyo kuhakikisha inasaidia watanzania hasa walioko katika kaya masikini nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujikwamua katika hilo.
TASAF inausimamiwa na kuutengewa fedha na Serikali pamoja na kupata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani (USAID) na Serikali ya Uhispania (Spain).
Lengo kuu la mfuko huu ni kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini kuinua hali zao za kimaisha kwa kuanzisha shughuli zitakazoinua uchumi wao kupitia taasisi kuanzia ngazi ya kikundi na hatimae vikundi vitaunda jumuiya na hata kuunda shirikisho la kuwakomboa.
Mfuko huo umekuwa na awamu kuu tatu mpaka sasa za kuwezesha kaya masikini Tanzania kujikwamua kiuchumi. Baada ya kukamilika kwa Awamu ya I na ya II, TASAF imeleta mafanikio makubwa kwa pande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Kwa kuwa jamii masikini zimewezeshwa kutekeleza miradi zaidi ya13,954 ( kwa awamu ya Kwanza miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni 1,704 na Awamu ya Pili jumla ya miradi 12,250 ilikamilika).
Serikali imeendelea na jitihada za kupunguza umaskini kwa kusimamia utekelezaji wa Awamu ya II na III ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kuhamasisha jamii yenye kipato cha chini kujiwekea akiba na kuwekeza.
Kupitia Mpango huo, jumla ya vikundi 1,620 vyenye wanachama 20,869 kwa upande wa Tanzania Bara na vikundi 158 vyenye wanachama 1,843 kwa upande wa Zanzibar viliundwa na kupewa mafunzo na hivyo kuwekeza.
Mbali na Taasisi mbalimbali zilizokuwa zikiwafikia na kuwasaidia wananchi katika hili ukiwemo Mfuko wa TASAF na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita) lakini bado kuna kazi kubwa ya kuwafikia wananchi masikini.
Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango aliwasilisha mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021, ambao utajielekeza katika dira ya Taifa ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Alisema mpango huo wa maendeleo wa miaka mitano unalenga katika ukuaji wa viwanda vitakavyo chochea mabadiliko ya uchumi na maendeleo ya watu kufikia uchumi wa kati wa viwanda na kuwa na watu wenye ujuzi watakao chochea ukuaji wa uchumi huo.
Aidha, alisema Serikali itajikita katika kupunguza umasikini, kutengeneza nafasi za kazi zitakazotokana na uboreshaji wa kilimo, mifugo na viwanda huku akisisitiza nidhamu, kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mazoea.
Alifafanua kuwa Serikali itahakikisha kuna elimu bure, huduma bora za afya na upatikanaji wa maji safi na salama, mambo yatakayo imarisha nguvu kazi ya Taifa na kufikia lengo lililo kusudiwa.
Waziri Dkt. Mpango aliwataka washirika wa maendeleo kusaidia juhudi hizo za Serikali katika mpango wa miaka mitano na zaidi kwa kuwa anaamini kwa upande wa Serikali imejidhatiti kupambana na vikwazo vinavyokwamisha kufikia lengo hilo kama rushwa, kukosa uwajibikaji na suala la utawala bora.
Mbali na hayo, Serikali imejiandaa kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati cha kampeni ya uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 2015 kwa kukipa kila kijiji nchini Sh milioni 50 katika mwaka wa fedha wa 2016-2017.
Akizungumza hivi karibuni Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shiliingi 59 bilioni za Kitanzania kwa lengo la utekelezaji wa ugawaji wa shilingi 50 milioni kila kijiji nchini.
Waziri Mkuu alisema mradi huo unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutenga fedha hizo kwa kila kijiji kuwa na mfuko wa uwekezaji kwa ajili uya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa.
Wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo mjini Dodoma,Naibu Waziri Ofisi ya Rais Sera, Uratibu, Bunge la Walemavu, Antony Mavunde alisema kuwa ahadi ya Rais Magufuli ya kila kijiji kupewa Sh milioni 50 itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2016-2017.
Alisema kuwa utaratibu wa kugawa fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Pamoja na mikakati yote hiyo vigezo ambavyo vimekuwa vikitumika katika kutoa mikopo na mitaji kwa vijana ni umri usiozidi miaka 35 ambavyo ni kujiunga na Saccos za vijana za wilaya na kuunda vikundi na kuvisajili kisheria,” alifafanua Naibu Waziri huyo.
Aidha, alisema ili kuhakikisha vijana wanakuwa wajasiriamali na wanaweza kupatiwa mikopo na mitaji, serikali imejiwekea mikakati ya kutambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana.
Wito kwa wananchi wote kwa ujumla kushirikiana kujitoa kwa dhati na kuzisimamia rasilimali fedha zitolewazo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa ya kupambana na umaskini nchini.
Post a Comment