TAASISI YA GRACA MACHEL MDAU MUHIMU WA ELIMU YA MTOTO WA KIKE NCHINI, IKIWA NA LENGO LA KUIELIMISHA JAMII.
Na Eleuteri
Mangi
Mtoto huanza
kujifunza kulingana na mazingira yake yanayomzunguka, mafunzo hayo
yanamuwezesha kupata uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa
kimaumbile ili aweze kuyamudu mazingira yake.
Hali hiyo inajenga dhana ya kupata elimu
kulingana na mazingira ambayo hujulikana kama elimu isiyo rasmi.
Ni vema ikaeleweka kwamba tunapozungumza
kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili, yaani watoto wa kike na wale wa
kiume. Katika hali halisi ndani ya maisha ya kijamii, elimu ni nyenzo ambayo
hutumiwa kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi
kingine bila kujali jinsia.
Elimu kwa watoto wa kike ni moja ya njia
bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania.
Manufaa hayo ya elimu kwa watoto wa kike
yanaweza kuonekana kwa mtu binafsi, familia zao, jamii yote na taifa kwa
ujumla.
Ni dhahiri, manufaa yanayopatikana kupita
elimu ni mengi katika jamii ikiwemo kupunguza idadi ya watoto ambao wanawake
hujifungua, kupunguza idadi ya vifo vya watoto wadogo, kupunguza idadi ya vifo
vya akina mama, kuwalinda dhidi ya maambukizo ya VVU/UKIMWI na kuongeza idadi
ya wanawake wenye kazi na mapato ya juu ambayo hudumu kwa vizazi vingi.
Hakika ukimuelimisha mtoto wa kike,
umemsaidia kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi bora kwa manufaa yake, familia yake
na hata taifa.
Hali hii imechukua sura mpya nchini
Tanzania ambapo Serikali, watu binafsi, mashirika ya dini na
taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha
mtoto wa kike anapata elimu ambayo ndiyo kinga na urithi pekee ambao hawezi
kunyang’anywa wala kugawana na mtu mwingine ndani ya familia na hata jamii
inayomzunguka.
Sura hiyo mpya imeoneshwa na Mfuko wa
Graca Machel (Graca Machel Trust) ambao umejikita katika kusaidia wanawake na watoto
nchi kadhaa Barani Afrika.
Taasisi hiyo imebisha hodi na kukaribishwa
nchini Tanzania mkoa wa Mara ambapo imeazimia kuwasaidia watoto wa kike 20,000
ndani ya mkoa huo ambao watanufaika kwa fursa ya kupata elimu.
Mapema Aprili 6, 2016 Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George
Simbachawene alibainisha Mfuko wa Graca Machel umeamua kuwasaidia watoto wa
kike wa mkoa wa Mara mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mama Graca
Machel alipomtembelea ofisini jijini Dar es salaam.
Moyo huo na juhudi za kusaidia watoto wa
kike ni wa kizalendo ambapo Waziri mwenye dhamana na tawala za mikoa
Simbachawene anasema “Ni fursa nzuri ya kushirikiana na wadau wa ndani na nje
ya nchi kuwasaidia watoto wetu wa kike kielimu ambayo itawasaidia kutoka katika
jamii ya umasikini na kuhakikisha wamepata fursa ya kuvuka umri wa vishawishi
na maamuzi yasiyo sahihi bila shida na pingamizi lolote”.
Watoto hao wanaotarajiwa kunufaika na
Mfuko huo mkoani Mara watatoka katika shule 104. Hatahivyo mfuko huo
unatarajiwa kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi mara baada ya kuanza kutoa
huduma hiyo mkoani humo.
Fursa hiyo adhimu na ni ya kuungwa mkono
hasa na wadau wa elimu mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla kwani kwa Mama Machel
haikuwa lazima kuichagua Tanzania, bali hekima na busara yake inatokana
ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji kwa kuzingatia mchango
mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo tangu awali.
Uhusiano huo mzuri uliopo kati ya nchi
hizo mbili ni wa kihistoria kwani pamoja na harakati za ukombozi Kusini
mwa Afrika, wananchi wa nchi hizo walishirikiana katika shughuli mbalimbali
chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano katika biashara na tamaduni kwenye
miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na Mtwara kwa upande wa Tanzania na katika miji ya
Chilimbo, Tete, Pemba na Sofala nchini Msumbiji.
Jambo jema hakika ni lazima kusifiwa na
kushangiliwa ili liweze kufana na kuwa na manufaa mengi zaidi, ndio maana
Waswahili husema “Chanda chema huvishwa pete”.
Mama Machel amekuwa mfano mwema wa
kuigwa maana anajali, anathamini na anatambua mchango wa mkoa Mara katika
historia ya maisha yake na nchi yake kwa kuwa ndio mkoa alipozaliwa Mwasisi wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeongoza harakati za ukombozi Kusini
mwa Afrika.
Ndiyo maana Mama Machel anasisitiza kwa
kusema “Lengo ni kuwabakisha watoto wa kike shuleni ili wapate elimu, ni lazima
tusaidiane wote, tuna kila sababu ya kusaidiana”.
Alipokuwa mkoani Mara katika chuo cha
ualimu Tarime mapema Mwezi Aprili mwaka huu, Mama Machel ameitaka
Tanzania kuwa na mpango wa utekelezaji katika kuhakikisha wanashughulikia
changamoto ambazo zinaweza kuwa sababu za mimba za utotoni kwa wasichana.
Mama Machel alisema kuwa iwapo
Tanzania na nchi nyingine za Afrika watu wataungana kwa pamoja kila mtu
atimize wajibu wake kwa nafasi yake, kwa utaratibu huo wa kujipanga ili
kusaidia kundi hilo la wasichana ni hakika mambo yaliyoko mbele yatafanyiwa
kazi vilivyo na ndoa za utotoni zitatokomezwa.
Mama Machel alisema kuwa watoto wa kike
wanatakiwa kupata nafasi ya kusoma na sio kuolewa wakiwa na umri mdogo, hivyo
Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha inakuwa bega kwa bega kuhakikisha
mtoto wa kike anapata haki zake za msingi zikiwamo za elimu.
“Katika mapambano yoyote, kitu kikubwa na
cha msingi ni elimu! Elimu pekee ndiyo itamaliza mila zote potofu tutafute
mbinu mbadala kuhakikisha watoto wanasoma, walimu wawe ni waangalizi wa watoto,
asipofika shule mzazi aulizwe maana watoto wote wanajulikana wanakotoka,
tunahitaji tuongeze idadi ya watoto wafike hadi elimu za juu”alisema Mama
Machel.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Magesa Mulongo
alimshukuru Mama Machel kwa moyo wake wa kizalendo kwa kuupa heshima mkoa huo
kupitia taasisi hiyo.
Akiwa mkoani Mara, wilayani Tarime Mama
Machel alisisitiza jamii iondokane na suala la ukatili wa kijinsia
ukiwamo ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni kwa lengo la kumlinda mtoto wa kike
na kumpa nafasi ya kutimiza ndoto zake.
Hatua hiyo ilitokana na Mama Machel
kujionea hali ilivyokuwa katika Shule ya Msingi Masanga ambapo alizungumza na
wananchi, wanafunzi na mabinti waliokimbia ukeketaji katika msimu wa tohara na
kuhifadhiwa kwenye Kituo cha Termination Of Female Genital Multilation (TFGM)
Masanga wilayani Tarime mkoani humo ambacho kimeanzishwa na Kanisa Katoliki katika
kumuokoa mtoto wa kike na maswahibu ya minyororo ya mila na desturi zisizofaa.
Katika kuthamini na kuupokea kwa vitendo
mchango wa Mama Machel, Serikali, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa
Mara wamesaini mkataba wa kutekeleza ili kuhakikisha watoto wa kike wanapata
elimu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa dhana ya
mtoto wa kike kuchunga mifugo zifutiliwe mbali, kila taasisi imepewa jukumu
lake, Serikali kupitia mkoa na halmashauri, Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) viongozi wa dini na wananchi.
Pande hizo kila mmoja wamesaini pamoja
mkataba wa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa kuziweka pembeni imani
potofu ambazo ndio zimekuwa kikwazo kwa mtoto wa kike kupata elimu.
“Halmashauri wanawajibu wa kuhakikisha
watoto wanaotambuliwa na wasitoroke katika vituo na shule wanaposoma, Wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na TAMISEMI wajibu wao ni kuandaa sera
zinazombeba msichana asitoroke shuleni, wajibu wa Serikali za mitaa na
vitongoji ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu wakati mkoa
jukumu lake ni kuhakikisha unafanya uratibu wa wadau wote wanahakikisha mtoto
wa kike anapata elimu” alisema Mulongo.
Mtazamo huo wa Serikali na wadau wengine
wa elimu unaungwa mkono na Mwakilishi wa Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu la
Umoja wa Mataifa (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem ambapo aliwahimiza watoto walio
katika kituo cha Masanga kutokata tamaa bali waweze kushikilia msimamo wa ndoto
zao kwa kushirikiana na wazazi waliopata mabadiliko katika kupinga vitendo vya
ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kuwa mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka
wa matumaini baada ya wazee wa mila kusema wameondokana na vitendo vya
ukeketaji ikiwa ni pamoja na wavulana kufanyiwa tohara.
Mwakilishi huyo alisema vyombo vya
kisheria vya mahakama pamoja na polisi vitaendelea kupewa mafunzo juu ya
kupinga vitendo hivyo kwa lengo la kuvikomesha kabisa.
“Tanzania ni nchi ndogo na idadi ya watoto
waliochini ya miaka 17 ni nusu ya Watanzania kwa hiyo hatuna budi kuwalinda
watoto hao kwa kuwapenda na kuwathamini,”alisema Dk Kanem.
Juhudi hizo za elimu kwa mtoto wa kike
zinachagizwa na Serikali Tanzania ambayo imekusudia kuleta mapinduzi ya
kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kusudio hilo la Serikali linaongozwa na
Sekta ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo kwa kwa mujibu wa Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa
2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu
kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda
kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa
kati na shindani ifikapo mwaka 2025.
Sera hiyo mpya imeweka dira ya elimu na
mafunzo nchini ambayo inayojali jinsia zote kupata elimu kwa usawa na kusimamia
nchi iwe ya maendeleo endelevu.
Dira hiyo inasimamia uhalisia “Mtanzania
aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili
kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa” anapaswa kuzingatia utaifa
kwanza.
Ili kuhakikisha elimu inawafikia watoto
wote, Serikali imeweka bayana katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014 yenye lengo la
kuwa na usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo. Pia Serikali itashirikiana
na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo
unazingatiwa.
Hapa nchini taasisi binafsi zimekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu licha ya mazingira
magumu aliyonayo.
Miongoni mwa taasisi za kupongezwa na
kuigwa mfano kutokana na kutoa umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu ni ya
Graca Machel Trust, Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mke wa Rais
Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Mama Salma Kikwete, taasisi ambayo
inasimamia Shule ya Sekondari WAMA–Nakayama iliyopo Kijiji cha Nyamisati Wilaya
ya Rufiji, Mkoa wa Pwani na Shule ya Sekondari ya WAMA- Sharaf iliyopo Mitwero
katika Manispaa ya Lindi.
Taasisi nyingine inayosimamia na kutoa
elimu kwa mtoto wa kike ni Mama Clementina Foundation (MCF) yenye makao yake
makuu mkoani Kilimanjaro inayoongozwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Shule ya
Sekondari Weruweu Dkt. Maria Kamm.
Taasisi ya MCF inatoa elimu kwa mtoto wa
kike kupitia shule za Kilimanjaro Academy iliyopo mjini Moshi mkoani
Kilimanjaro na shule ya sekondari ya Wasichana MCF Makambako iliyopo
Makambako.
Katika harakati za kuhakikisha mtoto wa
kike anapata elimu bora ili aweze kujitegemea, kujenga familia bora na kuwa
mchango chanya katika kujenga taifa imara kiuchumi, taasisi hizo zimeonesha
njia ya kuwa nuru ya mtoto wa kike katika kupata elimu.
Sera ya elimu nchini, inasisitiza uwiano
wa uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya msingi kwa wavulana na wasichana
uwe takribani 1:1, elimu ya sekondari uwe ni 1:0.9 wakati elimu ya juu ni 1:2.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwendelezo
wa idadi ya wanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi inayofuata kwa wasichana
uwiano huo umekuwa ukipungua.
Ingawa kiwango cha mdondoko kinaathiri
wavulana na wasichana, tathmini inaonyesha kuwa wasichana wana uwezekano mkubwa
zaidi wa kukatisha masomo hususan wanapofikia katika madarasa ya juu kuanzia
darasa la tano.
Ndiyo maana taasisi za Graca Machel, WAMA
na MCF zimeona kuna umuhimu wa kumsomesha mtoto wa kike kwa ushiriki katika
fursa za elimu na mafunzo hatua ambayo itawasaidia wasichana kupata nafasi za
usimamizi na uendeshaji katika sekta mabalimbali nchini.
Kwa taarifa za mwishoni mwa mwa 2015 jumla
ya wanafunzi 503,914 kati ya wanafunzi 518,034 waliofaulu kujiunga na kidato
cha kwanza mwaka 2016.
Ki uhalisia, idadi ya wanafunzi
waliojiunga kidato cha kwanza mwaka huu sawa na asilimia 97.3 ambao wamepata
nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali.
Ili kuhakikisha wanafunzi hawa wanapata
elimu inayotarajiwa Serikali imetenga Sh. bilioni 131 kwa ajili ya shughuli za
uendeshaji shule, chakula kwa wanafunzi wa bweni na fidia ya ada ya mitihani
kwa kipindi cha kuanzia mwezi Desemba mwaka huu hadi Juni mwaka 2016.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, alisema kati ya wanafunzi
waliochaguliwa, wasichana ni 255,843 sawa na asilimia 99.2 na wavulana ni
248,076 sawa na asilimia 97.7
Sura hiyo inaonesha idadi ya wasichana
waliojiunga kidato cha kwanza ni kubwa kuliko ya wavulana kwa zaidi ya asilimia
1.5, ongezeko ambalo linaonesha kuwa Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya uelewa
wa kumpatia elimu mtoto wa kike.
Siyo wanafunzi wote wanaomaliza shule ya
msingi, kidato cha nne na kidato cha sita wanajiunga na shule za Serikali, ndio
maana taasisi nyingine zinatoa mchango wao katika kuhakikisha watoto wa kike
nchini wanapata elimu katika ngazi mbalimbali.
Hatua hiyo ya Tanzania inaungwa mkono na
mataifa duniani ndio maana ikaanzishwa Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ili
kutambua haki za watoto wa kike na kuimarisha jitihada za kimataifa za
kutokomeza unyanyasaji, ubaguzi na ukatili wa kijinsia na tofauti ya fursa za
kiuchumi zinaowaathiri zaidi watoto wa kike.
Takwimu zinaonyesha kuwa nchi
zinazowaelimisha watoto wa kike kwa usawa huwa na ustawi na maendeleo makubwa
zaidi.
Kwa kuwapa watoto wa kike mwaka mmoja wa
ziada wa masomo baada ya muda wa wastani katika elimu ya msingi utawaongezea
kati ya asilimia 15 na 20 ya kipato chao na mwaka mmoja wa ziada katika elimu
ya sekondari utaweza kumuongezea mtoto wa kike kipato chake kwa kati ya
asilimia 15 na 25.
Aidha, watoto wa kike walio soma hukawia
zaidi kuolewa na kupata watoto, Hali kadhalika, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa
wasichana waliopata elimu hapo baadaye kuwa na watoto wenye afya njema na ambao
pia watapata elimu nzuri.
Ndio maana Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali
ya Awamu ya Nne Mama Kikwete aliwahi kusema “……. Mtoto wa Mwenzio ni mwanao,
tunamaanisha sote tunapaswa kuwajibika kwa ajili ya ulinzi na ubora wa maisha
ya watoto toka wakiwa tumboni hadi wanapozaliwa na kusimamia maadili yao
wanapoendelea kukua”.
Mama Salma alitoa msisitizo kwa Watanzania
na kuwaasa waache kulaumiana juu ya maadili ya vijana, na kuwaomba
warejee malezi ya wazee ili kila mmoja awajibike kumuona mtoto wa mwenzake kuwa
ni wa kwake na kumrekebisha pale anapokosea.
Ni wajibu wa kila mpenda maendeleo kujua
kuwa ni fursa ya pekee kumuelimisha mtoto wa kike wajibu na dhamana ya jamii
kutambua ukimuelisha mtoto wa kike ni kuelimisha jamii nzima.
Ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu ya
kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8
imesisitiza kuwa “Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote”
Post a Comment