KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI AFUNGUA MDAHALO WA VIJANA KUJADILI HATMA YA AJIRA KWA VIJANA NCHINI
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
akifungua mdahalo wa hatma ya ajira kwa vijana wa Tanzania ulioandaliwa na
Shirika la Kimataifa la Ajira (ILO) na kushirikisha vijana kutoka Tanzania Bara
na Visiwani leo jijini Dar es Salaam
Na Anitha Jonas
mwambawahabariblog
Vijana wametakiwa
kugeuza changamoto kuwa fursa na kuwa na utamaduni wa kujiajiri na kuchapa kazi
kwa bidii badala ya kusubiria kuajiriwa huku wakilaumu mamlaka zinazoshughulika
na vijana nchini.
Hayo yamesemwa
na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof.
Elisante Ole Gabriel alipokuwa akifungua Mdahalo wa siku mbili kujadili
Hatma ya Ajira kwa Vijana Tanzania uliyoandaliwa na Shirika la
Kimataifa la Ajira (ILO) leo jijjni Dar es Salaam.
“Changamoto ya
ukosefu wa ajira inaweza kutumika kama fursa kwa kijana anayejitambua kwa kuwa
na fikra chanya itakayomuwezesha kutumia elimu aliyoipata kujiajiri bila kuona
aibu kufanya baadhi ya kazi mbali ya kuwa amesoma hadi elimu ya juu hivyo
kujiongezea kipato,”alisema Prof. Gabriel.
Akizungumza na
vijana hao Prof. Gabrieli amesema kuwa utafiti wa mwaka 2012 kuhusu
idadi ya vijana nchini ulionyesha kuna vijana takribani 16.2 Millioni
nchini, na kati ya hao vijana walioajiriwa katika Sekta ya Umma ni Vijana
188,000, Sekta Binafsi Milioni Moja, waliojiajiri wenyewe ni 1.1 millioni
na waliojiajiri katika sekta ya Kilimo ni vijana 13.2 milioni.
Aidha Prof. Gabriel
amesema kuwa vijana wanatakiwa kujitahidi kukimbizana na teknolojia kwani
ukuwaji wa utandawazi katika ulimwengu sasa umekua wa kasi hivyo
kupambana kukabiliana na changamoto hiyo katika soko la ajira.
Kwa upande wa
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Ajira (ILO) nchi ya Tanzania,
Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda Bi. Mary Kawar amesema kuwa shirika hilo liko
tayari kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya ajira ili kupunguza tatizo la
ukosefu wa ajira kwa vijana.
Naye mshiriki wa
mdahalo huo Bw. Masson Kimbo ameiomba serikali kupitia mifumo ya elimu nchini
itakayowawezesha vijana kujengewa uwezo wa kujiajiri na kuwa na fikra pana
katika masuala ya ujasiriamali.
Post a Comment