JESHI LA POLISI LATOA TAARIFA KUHUSU UTAPELI WA AJIRA KATIKA TAASISI MBALIMBALI
Katika siku za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali hapa
nchini, kumejitokeza makundi ya watu ama mtu binafsi kutumia mwamvuri wa
taasisi fulani kujipatia kipato kwa njia za udanganyifu (utapeli) kwa kuwaahidi
vijana kwamba watawapatia ajira katika taasisi hizo.
Makundi haya ya kihalifu imebainika kwamba yapo katika maeneo
mbalimbali, hivyo, ni suala ambalo linahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa
wananchi ili kukomesha vitendo hivyo.
Juhudi za makusudi zinaendelea kufanyika na jeshi la polisi ili
kuwatia mbaroni watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kitapeli.
Aidha, kufuatia kuibuka kwa vitendo hivyo, tayari Jeshi la
Polisi limewakamata matapeli wawili wakiwa wamekusanya vijana katika mikoa ya
Kilimanjaro na Mbeya, uchunguzi dhidi yao unaendelea na pindi utakapokamilika
watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabiri.
Jeshi la Polisi likishirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na
Usalama, kimsingi, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na Ulinzi na
Usalama imara.
Tutaendelea kupambana na makundi haya ya kihalifu na
utapeli ili nchi yetu iendelee kuwa salama.
Tunawasihi wananchi kufuatilia taarifa kwenye vyanzo sahihi juu
ya jambo lolote wanalotaka kulifanya ili kuepuka utapeli unaoweza kufanywa na
baadhi ya watu kwa lengo la kujipatia vipato.
Aidha, wananchi watoe taarifa kwenye vyombo vya usalama kuhusu
tabia na mienendo yoyote wanayoitilia mashaka.
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vyote vya Ulinzi na
Usalama viko imara, makundi ya kiuhalifu na wahalifu wote wajue hawana pa
kukimbilia, watakamatwa.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.
Post a Comment