HOTUBA YA KIONGOZI WA CHAMA CHA ACT WAZALENDO NDGUGU KABWE Z R ZITTO KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CHAMA ILIYOKETI JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 25 APRILI 2016
mwambawahabariblog
Ndugu Mwenyekiti wa Chama,
Ndugu Makamu Wenyeviti wa Chama,
Ndugu Katibu Mkuu
Ndugu wajumbe wa Kamati Kuu
Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa
Mabibi na Mabwana:
Leo tunakutana miezi sita baada ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na takribani mwaka mmoja tangu tuzindue rasmi Chama
chetu kinachopigania kujenga siasa na jamii ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Aidha,
leo tunakutana tukikaribia mwaka mmoja tangu tuzindua Azimio la Tabora ambapo
tulidhamiria kuhuisha Azimio la Arusha ambalo mwakani linatimiza miaka 50 tangu
litangazwe na Chama cha TANU kule mjini Arusha. Aidha, na muhimu Zaidi,
tunakutana miaka miwili tangu chama chetu kiliposajiliwa rasmi. Nawapongeza
Kamati ya Maendeleo ya Jamii kwa kuandaa maadhimisho ya wiki ya chama kuanzia
tarehe 1 Mei 2016.
Tangu tulipokutana Tabora mpaka leo
kuna mambo mengi sana yametokea ikiwemo Uchaguzi Mkuu ambao umewezesha Chama
chetu kupata uwakilishi Bungeni na kuongoza Halmashauri ya Manispaa Kigoma
Ujiji na uwakilishi kwenye Halmashauri za Wilaya 11 nchini. Chama chetu kimekua
na sote kwa pamoja tujipongeze kwa hatua kubwa tuliyopiga.
Katika kujipongeza kwetu kuna watu
mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wametusaidia kufika hapa tulipo.
Wengine wametangulia mbele ya haki, akiwemo Ndugu yetu Mzee Estomih Malla
aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na mgombea wa Ubunge katika Jimbo la
Arusha Mjini, na wengine katika ngazi mbalimbali za chama. Viongozi wetu wa
chama katika ngazi za kuanzia matawi, kata na majimbo; katika ngazi ya mkoa na
Taifa walijitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kukifanya chama kisonge mbele na
kupanda mbegu. Nachukua fursa hii kuwapongeza wote kabisa na kuwashukuru kwa
kazi kubwa mliyofanya. Kwa namna ya kipekee kabisa nampongeza Mgombea wetu wa
Urais, Mama Anna Elisha Mghwira na Mgombea Mwenza wake Ndugu Hamad Yusuf, kwa
kuzunguka nchi nzima kukitangaza chama chetu na kukiweka katika ramani ya siasa
nchini. Kazi haijaisha, lazima iendelee ili kuweza kutimiza malengo yetu ya
kujenga siasa mpya katika nchi yetu, siasa za masuala na kuachana kabisa na
siasa za matukio. Katika uchaguzi uliopita tulipenda mbegu na ikaota. Kazi
kubwa tuliyo nayo sasa ni kuilea mbegu hii na kuhakikisha kwamba inakua kwa
kasi ili hatimaye mwaka 2020 chama chetu kiweze kuchukua usukani wa kuongoza
nchi yetu. Mpango Mkakati mtakoujadili na kuupitisha leo
umeanisha kwa kina namna ya kuilea na kuikuza mbegu hii.
Timu yetu ya Watendaji wa Makao Makuu
ya chama na Vikao vya Halmashauri Kuu tayari vimepitisha Mpango Mkakati kwa upande wao na sasa ni zamu ya
Mkutano huu wa Halmashauri Kuu kujadili na kupitisha Mwelekeo wa Chama chetu
katika Miaka mitano ijayo. Kama myakavyoona, Kauli Mbiu yetu mpya
inayopendekezwa ni SIASA ni MAENDELEO (Developmental Politics). Tunataka
tujihangaishe na mambo ya wananchi, kero za wananchi, changamoto za wananchi na
kushiriki nao kupata mawajawabu ya Changamoto hizo. Tunataka kila mahala ambapo
Chama chetu kimepata uwakilishi kuongoza tofauti na vyama vingine; kuonyesha
kuwa kweli tunataka kufanya siasa tofauti. Kila Mtaa ambao ACT Wazalendo ina
Mwenyekiti au mjumbe, kila Kijiji ambacho tunaongoza na kila Kata ambayo tuna
Diwani, lazima iwe tofauti kimaendeleo na kiuwakilishi. Kila Mamlaka ya
Serikali ya Mtaa ambayo tunaongoza tuonyeshe tofauti na Mamlaka ambazo wenzetu
wanaongoza. Tujikite kwenye mambo ya wananchi. Ndio Siasa ya Ujamaa inataka
hivyo.
Hali ya Nchi yetu Kisiasa, Kiuchumi na
Kijamii
Kisiasa
Hivi sasa nchi yetu ina Serikali mpya.
Rais ameanza kazi kwa kasi kubwa katika eneo moja muhimu sana ambalo lilikuwa
moja ya msingi mkubwa wa kuanzishwa chama chetu – kupambana na ufisadi. Rais
anaita ‘kutumbua majipu’. Chama chetu kilimuunga mkono Rais katika hatua ya
mwanzo kabisa katika jambo hili. Ninaamini kuwa bado tutaendelea kumuunga mkono
kwani ufisadi ni kansa na ni lazima kwanza kuizuia isisambae na kisha kuanza
kuitibu kabisa. Hatua ambacho zinachukuliwa sasa na Rais ni hatua muhimu sana
katika kuondoa ‘kutogusika’ kwa baadhi ya watu katika nchi yetu. Mnamkumbuka
wakati tunazindua Chama tulizungumzia kuhusu ‘cartels’ - vikundi maslahi ambavyo vimeshika
uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo, tunasema kuwa bado Rais hafanyi inavyopaswa.
Bado Rais anapapasa suala la Ufisadi. Kuna mambo ya muda mrefu ambayo
tunaendelea kama nchi kuyalipia Rais ameyakalia kimya. Mfano ni suala la Tegeta
Escrow. Bado Mtambo wa IPTL upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali
inawalipa matapeli hawa zaidi ya Tshs. 8 bilioni wazalishe au wasizalishe
umeme. Hivi ndio vikundi maslahi ama cartels katika sekta ya Nishati ambavyo
bila kuvibomoa Rais ataonekana anachagua katika vita hii.
Suala la HatiFungani ya dola za
kimarekani 6 milioni. Ni kweli kwamba kuwa kuna watu tayari wamefikishwa
mahakamani kwa rushwa ya dola milioni sita. Lakini Serikali imefisha inaowaita
madalali wa rushwa hiyo. Walioitoa rushwa hiyo Benki ya Standard ya Uingereza
haipo mahakamani. Waliopokea rushwa hiyo maafisa wa Wizara ya Fedha hawapo
mahakamani. HatiFungani hii ambayo Serikali imeanza kulipa riba yake ni ghali
mno na imeongeza Deni la Taifa kwa kiwango cha shilingi 1.2 trilioni bila ya
riba. Itakapofika mwaka 2020 ambapo tutakuwa tumemaliza kulipa deni hili,
tutakuwa tumelipa zaidi ya shilingi 1.8 trilioni, shilingi bilioni 600 zaidi!
Watanzania zaidi ya 2000 duniani kote wameweka saini kutaka Taasisi ya Rushwa
kubwa nchini Uingereza ( SFO ) kufungua upya shauri hili na kuitaka Benki ya
Standard iwajibike kwa ufisadi huu dhidi ya nchi masikini kama yetu.
Rais wetu angeongoza Watanzania kukataa
mikopo ya namna hii ambayo inafukarisha nchi ingekuwa ni hatua kubwa sana.
Lakini TAKUKURU wanaona ni sifa kuweka ndani watu kwa bilioni 12 bila
kutuwaambia watu watakaofaidika na bilioni 600 zaidi tutakazolipa katika deni
hili. Ndio naama tunasema Rais na Serikali yake bado hawafanyi ya kutosha
katika vita dhidi ya rushwa. Sio suala la kutumbua majipu tu, ni suala la
kuweka mfumo madhubuti ambao utazuia rushwa kabisa.
Chama chetu cha ACT Wazalendo ni lazima
kiendelee kuunga mkono juhudi zozote za kuondoa ufisadi nchini kwetu. Hata
hivyo Chama chetu ni lazima kiendelee kukosoa Serikali pale ambapo tunapoona
mambo hayaendi sawa. Tusiogope kuikosoa Serikali kwa hoja kwani kukosoa
Serikali ni tukio muhimu sana la kizalendo.
Hivi sasa Wabunge wa vyama vya Upinzani
wamesusia Bunge kwa sababu kuu tatu. Moja ni Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja
na Televisheni ya Taifa na Televisheni Binafsi, mbili ni Matumizi nje ya mpango
wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge na tatu ni Serikali kutokuwa na ‘instruments’
kwa Mawaziri. Hoja hizi ni hoja za msingi sana. Ni Haki ya wananchi kuona moja
kwa moja namna ya wawakilishi wao wanavyofanya kazi. Censorship ni moja ya
dalili za kujenga udikteta nchini. Kwamba anayepaswa kuonekana moja kwa moja ni
mtu mmoja tu; inakuwa kama Korea Kaskazini hivi! Hili ni jambo ambalo Chama
chetu lazima kiungane na vyama vingine kulikemea kwani ukiliacha hatujui
kitafuata nini. Kwamba Bunge lina studio zake nk, ni jambo la kuhadaa tu
wananchi. Umeshawapa wananchi uhuru wa kuona Bunge moja kwa moja kwa miaka 10,
halafu leo unawanyang’anya? Mwalimu Nyerere alipata kusema “ jambo lolote
linalowapa uhuru wananchi ni jambo la kimaendeleo”. Suala la gharama ni hoja
dhaifu mno maana kampuni huru kama Azam TV na Startv walikuwa wanaonyesha bila
hizo gharama za Serikali. Ni lazima kushikamana na wenzetu katika jambo hili.
Suala la Matumizi kufanyika nje ya
Mfumo wa Bajeti ni suala la kisheria. Bajeti inaongozwa na Sheria mbalimbali
kama vile Sheria ya Fedha ( The Finance Act), Sheria ya Matumizi na Sheria ya
Fedha za Serikali ( Public Finance Act). Kuna taratibu za Fedha za Serikali
kuhamishwa kutoka fungu moja kwenda fungu jengine au ndani ya fungu husika.
Katika Sheria zote hakuna mahala Rais amepewa mamlaka ya kuhamisha fungu lolote
lile. Hivyo, hoja iliyotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya
Ujenzi kuongezewa fedha mara 4 zaidi ya fedha ilizotengewa na Bunge ni hoja
yenye nguvu sana. Izingatiwe kuwa Rais alikuwa Waziri katika Wizara iliyoongezewa
Fedha hizo. Sio hoja ya kupuuza. Tukipuuza leo Rais anaweza kuamua kufanya
lolote na nchi ikaingia kwenye taharuki. Lazima tumkatalie ili ajifunze kufanya
kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi yetu. Mwalimu Nyerere alipata
kusema “ Kuna mambo Rais akifanya, ya hovyo wananchi wakatae, awe Rais awe Rais
square”. Dhana ya Mamlaka ( Power) ni dhana ngumu sana, ukilamba bila kuzuiwa
utaendelea kulamba tu. Tumzuie Rais kupoka madaraka ya vyombo vingine vya dola.
Tumuunge mkono kutekeleza madaraka yake ya Urais lakini lazima tuhakikishe
kwamba haingilii mamlaka ya vyombo vingine.
Suala la ‘instruments’ ni suala
linaloendana na suala la matumizi kubadilishwa. Kimsingi bila instruments
Baraza la Mawaziri lina watu 2 tu – Rais na Makamu wa Rais. Kama Waziri Mkuu
hana instruments hakuna Waziri Mkuu. Kama Mawaziri hawana instruments, hakuna
mawaziri. Hivi sasa Serikali ina mawaziri hewa na hata maamuzi yao ni hewa.
Instruments ni jambo la kisheria. Ndio zinatoa mamlaka kwa Mawaziri kufanya
kazi. Hivyo kutokana na kutokuwa na Instruments kimsingi Rais ni Waziri wa
Wizara zote nchini hivi sasa. Natoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ahakikishe Mawaziri wanapewa instruments ili waweze kuwepo kisheria na maamuzi
yao yawe ya kisheria. Chama chetu kisikubali nchi kuendeshwa na mtu mmoja kwa
jina la Rais. Nchi yetu inaendeshwe kikatiba.
Hata hivyo nataka kuwaasa Wabunge
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge la 11 lazima liwe
tofauti na Mabunge yaliyopita. Mabunge yaliyopita yalikuwa na kazi ya kupambana
na ufisadi kwa sababu Serikali iliyopita ilionekana kutofanya kazi hiyo vizuri.
Bunge lilijipa kazi ya ‘kutumbua majipu’ na kuilazimisha Serikali kutekeleza
Maazimio ya Bunge. Hivi sasa kazi hiyo ya kutumbua majipu inafanywa na Serikali
yenyewe, inafanywa na Rais mwenyewe. Hivyo Bunge lazima litafute wajibu mpya
katika kipindi hiki. Bunge na hasa wabunge wa upinzani lazima sasa kutazama
njia mbadala za kuifanya Serikali iwajibike. Kwa mfano, ni dhahiri nafasi ya
wazi kabisa ni katika kuanisha mwelekeo wa nchi na kujenga mfumo madhubuti wa
uwajibikaji. Ni lazima kubadilika na kubadili aina ya siasa. Tusifanye mambo
yanayotarajiwa; kwa mfano kutoka tu bungeni halafu tunarudi tena. Kama Serikali
inaenda kinyume na sheria, katiba na kanuni, kwa nini tusifanye mikutano ya
wananchi, bunge la wananchi ambapo tunajadili kwa uwazi mambo yanayotusibu.
Tunaweza kutumia vizuri digital technology kuhakikisha ujumbe wetu unafika kwa
wananchi bila kujali kama TBC wanaweka live au la. Ni lazima tuwe innovative
katika Siasa. Tusifanye siasa za kila siku.
Kiuchumi
Serikali imewasilisha mpango wa Bajeti
ambapo inatarajiwa kukusanya na kutumia zaidi ya shilingi trilioni 29 katika
mwaka wa fedha 2016/17. Hii ni sawa na asilimia 28 ya Pato la Taifa ambalo sasa
ni shilingi trilioni 98. Hata hivyo kwa fedha zetu za madafu inaonekana ni
nyingi sana, kwani inatokana na kuporomoka kwa shilingi dhidi ya fedha za
kigeni hasa dola ya kimarekani. Hata hivyo ni Bajeti kubwa yenye ongezeko kubwa
hasa katika makusanyo ya ndani na mikopo ya ndani.
Serikali itaongeza wigo wa kodi na hata
kufikia wachuuzi wadogo wadogo kama wamachinga ili kuweza kupata fedha za
kutekeleza Lakini pia Serikali itakopa fedha nyingi sana kutoka nje ya nchi,
takribani shilingi trilioni 2. Aidha, serikali itakopa sana kwenye benki za
ndani na hivyo kufukuzana na wafanyabiashara katika mikopo ya ndani. Haya ni
mambo ambayo ni muhimu kuyatazama katika muktadha mzima wa uchumi wa nchi yetu.
Nina mashaka makubwa sana kama wachumi Serikalini waliikalia vizuri Bajeti
ianyopendekezwa kwani kuna maeneo ambayo yanatia mashaka makubwa.
Kwa mfano, Serikali inasema itaongeza
mapato wakati mapato katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje yameanza kushuka.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Benki Kuu ya Mwezi Februari 2016, mizigo kutoka nje
katika Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa 40%. Katika mazingira hayo na
kuzingatia kuwa tunategemea kodi ya forodha kwa asilimia 30 ya mapato yetu,
mapato yatashuka tu. Vilevile Serikali imeshindwa kuzingatia kuwa Uchumi wa
Dunia sasa unashuka na Uchumi wa Afrika unashuka. Tanzania sio kisiwa na
inategemea sana uchumi wa Dunia na hasa nchi kama China ambapo uchumi wao
umeporomoka sana. Chama chetu kiitake Serikali kuitazama upya Bajeti na
kuelekeza fedha za kutosha katika maeneo yatakayowezesha uzalishaji wa ndani na
hasa katika sekta ya kilimo ili kudhibiti kuporomoka kwa uchumi wa Dunia.
Kijamii
Hali ya wananchi ni mbaya; bidhaa
zimeanza kupanda bei kuliko ilivyokuwa kabla ya uchaguzi. Chama chetu kijadili
kwa undani hali ya maisha ya wananchi na kutoa tamko na mapendekezo ya namna ya
kukabiliana na hali hiyo. Hali ya huduma za afya na elimu bado ni mbaya na
hakuna mabadiliko makubwa ya ubora wa elimu na huduma za afya. Chama chetu
kishauri Wabunge kuwatazama wananchi katika michango yao Bungeni ili Bajeti ya
nchi yetu ihangaike na keri za wananchi.
Hitimisho
Ninawaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Chama muendelee kuwa wamoja na tuweze kujenga chama imara chenye kujali
shida za wananchi. Tuna wajibu mkubwa na uwezo wa rasilimali fedha mdogo licha
ya kwamba tuna rasilimali watu kubwa yenye kuweza kuleta mabadiliko. Ninawaomba
tusivunjike moyo bali tutumie kila tulichonacho kujenga chama chetu katika
misingi ya Ujamaa wa Kidemokrasia nchini kwetu. Nawatakia mkutano mwema.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Jumatatu 25 Aprili 2016.
Post a Comment