TRA YAONGEZA MWEZI MMOJA USAJILI WA PIKIPIKI
Mwambawahabariblogspot.com
Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) imesema imeongeza muda kwa
usajili wa vyombo vya usafiri vya Pikipiki za magurudumu mawili na
matatu mpaka Februari Mosi mwaka 2016.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Alphayo
Kidata alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika kikao chake cha
kutoa taarifa kwa umma juu ya ukusanyaji wa kodi, Kaimu Kamishna Mkuu amesema
wameamua kuongeza muda wa zoezi la usajili wa pikipiki ili kuiwapa nafasi wale
ambao bado hawajasajili.
“ Natoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya pikipiki kusajili vyombo
vyao mapema ili wasipatwe na adha itakayojitokeza baada ya muda uliotolewa
kumalizika ” Alisema Kaimu Kamishna Kidata.
Ameongeza kuwa zoezi hilo lilikumbwa na changamoto kadhaa
zilizowalazimu kuongeza muda mara mbili, ambazo ni umbali wa vituo vya usajili
na makazi ya wamiliki wa pikipiki hasa mikoani,pamoja na upotevu wa nyaraka za
kununulia pikipiki.
Aidha Kaimu Kamishna Alphayo Kidata ameomba wananchi kufungua
ukurasa mpya wa ushirikiano na Mamlaka ili kutimiza
azimio la Serikali ya Awamu ya Tano ya kulijenga taifa kwa kufanya kazi na hasa
kulipa kodi stahiki zinazoleta mapato yanayowezesha maendeleo katika taifa
letu.
Zoezi la usajili wa pikipiki lilianzishwa kwa lengo la kurahisisha
ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyombo hivyo, zoezi hili lilipangwa
kukamilika tangu Desemba 31 2015 lakini ikaonekana wengi hawakusajili pikipiki
zao hivyo basi Mamlaka imetoa mwezi mmoja mpaka Februari Mosi 2016 kwa wenye
Pikipiki kusajili.
Post a Comment