Ads

DCEA YAENDELEA KUDHIBITI MATENDO YA KIGAIDI KUPITIA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA

Na Francisco Peter, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeeleza kuwa imefanikiwa ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya nchini, hali inayochangia kupungua kwa vitendo vya kigaidi na uhalifu mwingine katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 9, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na mamlaka hiyo kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari. 

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, amesema kuwa katika maeneo mbalimbali nchini, matumizi ya dawa za kulevya hususan miongoni mwa vijana yamepungua kutokana na kuimarika kwa udhibiti na utoaji wa elimu kwa jamii.

Amesema kuwa kwa sasa si rahisi tena kupata dawa kama heroin mitaani, hali ambayo imesababisha baadhi ya watumiaji kugeukia unywaji wa pombe kupita kiasi kama mbadala wa kulewa. 

Hata hivyo, DCEA imeendelea kuchukua hatua za kutoa elimu kwa umma ili kukomesha matumizi ya dawa za kulevya nchini.

“Kwa sasa ukiingia mtaani si rahisi kuipata heroin. Badala yake, baadhi wameingia kwenye unywaji wa pombe uliopitiliza. Ndiyo maana mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Ameongeza kuwa matumizi ya dawa za kulevya huchochea vijana na jamii kwa ujumla kujikuta wakijihusisha na vitendo vya kigaidi na uhalifu, jambo lililoifanya DCEA kutumia mbinu mbalimbali za elimu na udhibiti ili kukomesha tatizo hilo.

Aidha, imeelezwa kuwa kwa sasa duniani kuna zaidi ya dawa mpya 1,400 za kulevya ambazo hutengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu. 

Dawa hizo hutengenezwa kwa lengo la kukwepa sheria, kwani dawa nyingi zinazojulikana tayari zimo kwenye orodha ya kisheria ya dawa zilizopigwa marufuku.

Kwa upande wake, Moza Makumbuli amesema kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu mpya za kukwepa sheria, ikiwemo kutengeneza dawa mpya ambazo bado hazijajumuishwa katika orodha ya dawa zinazokatazwa kisheria.

Ameeleza kuwa dawa hizo hutengenezwa na wataalamu wabobezi wa sayansi kwa kutumia kemikali bashirifu viwandani, jambo linalofanya ziwe ngumu kugundulika kwa haraka.

“Siku hizi dawa nyingi za kulevya zinatengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu. Japokuwa baadhi hazipo kwenye sheria bado ni dawa za kulevya na zina madhara makubwa,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, DCEA imetoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuendelea kutoa taarifa za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Imeelezwa kuwa mchango wa waandishi wa habari umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la matumizi ya dawa hizo, pamoja na kufuatilia taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ili ziweze kufanyiwa kazi na mamlaka husika.

No comments