WAANDISHI WA HABARI WAASWA MATUMIZI SAHIHI YA AI (AKILI MNEMBA) KUELEKEA UCHAGUZI
Na Angelina Mganga
DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA) kwa kushirikiana na taasisi ya GIZ toka Ujerumani wametoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuwafanya waandishi wa habari kuandika habari ambazo haziwezi kutweza utu wa mtu hasa katika kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi za uandishi wa habari kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo Mkurugenzi Msaidizi anaesimamia Kitengo Cha Miradi na Mikakati TAMWA,Sylvia Daulinge amesema kwamba ni muhimu waandishi habari kuandika habari sahihi na kufuatilia kwa makini habari za kweli ili kuepuka kutoa taarifa ambazo si sahihi(disinformation)
"Tafiti zinaonyesha taarifa tatanishi ni chanzo cha vurugu za kisiasa",alisema Daulinge
Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia elimu waandishi jinsi ya kuripoti taarifa sahihi bila kuumiza mtu ,kuvunja moyo na kukatisha tamaa.
Pia mafunzo hayo yalilenga kutoa elimu ya uelewa mpana kuhusu matumizi ya AI katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.
"Waandishi tumehimizwa kuwa makini sana katika zama hizi za kutumia AI,kufanya upembuzi wa kina kabla yakutoa taarifa tunazopokea ama kuziona mtandaoni kwa kuzifuatilia kwa karibu ili kuepuka taarifa tatanishi na ambazo hazi ukweli",amesema Nora Damiani
Kwa upande wake Mratibu wa Program toka Global Action for Peace building Initiative(GAPV#defyhate now Online GBV and Disinformation workshop,Njoki Kariuki amewataka waandishi kujiepusha na taarifa tatanishi na ambazo zinaleta migawanyiko katika jamii.
Aidha,amewataka wanahabari kufanya uchambuzi wa kina kutoka vyanzo mbalimbali vya habari wanapopokea taarifa"nani kasema Nini,kasema lini na wapi na kwa nini aseme hayo?",
Amesisitiza kwamba ni vema kusikiliza sera za mgombea bila kusambaza taarifa tatanishi zenye lengo la chuki ama zinazoweza kutweza utu wa mtu.
Katika kipindi hiki cha zama za matumizi ya teknolojia ,teknolojia inafanya taarifa kusambaa kwa haraka na kwa dakika chache kwahiyo ni muhimu kuongeza umakini wa hali ya juu .
AI ina manufaa makubwa endapo itatumika vizuri lakini pia inaweza kusababisha madhara kwa kusambaza taarifa potofu na za uchochezi.
Post a Comment