Njia salaama zawekwa wazi kuwaruhusu raia kuepuka mapigano nchini Ukraine
Kumeripotiwa maendeleo kidogo katika uwekaji wa njia salaama kuwaruhusu raia kuepuka mapigano nchini Ukraine. Pande mbili zilikubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa saa 12 siku ya Jumanne kupisha uhamishaji wa raia.
Jeshi la Urusi limefahamisha kuwa kuwa limeanza kutekelea usitishaji mpya wa mapigano nchini Ukraine na kufungua njia za kiutu katika miji mitano.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov, alisema usitishaji mapigano umeanza asubuhi, na njia salaama zitafunguliwa kwa raia kutoka miji mikubwa ya Kyiv, Chernigov, Sumy, Kharkiv na Mariupol.
Licha ya mapatano hayo, maafisa wa Ukraine wanasema ndege za Urusi zimeendelea kushambulia miji ya mashariki na kati mwa Ukraine usiku kucha. Makombora yalipiga viunga vya mji mkuu, Kyiv.
Kwa mujibu wa maafisa wa Moscow, sehemu kubwa ya njia hizo zitaelekea Urusi, ama moja kwa moja au kupitia Belarus.
Lakini Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa alisema njia za kiutu kutoka mji mkuu Kyiv na miji mingine zinaweza kuwapa watu chaguo la wapi wanataka kwenda.
Mwanaume akimsaidia mwanamek anaeondolewa kuvuka daraja lililoharibiwa wakati mwanamke huyo na wengine wakiondoka mjini Irpin, kaskazini-magharibi mwa Kyiv, Machi 7, 2022.
Maafisa wa Ukraine na Urusi walifanya duru ya tatu ya mazungumzo y amoja kwa moja jana Jamatatu, tangu kuanza kwa uvamizi Februari 24, na kwa mujibu wa wanadiplomasia wa mataifa hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo mawili wanatarajiwa kukutana nchini Uturuki siku ya Alhamisi.
Rais Volodymyr Zelenskiy amewahimiza raia wake kuendelea kupinga uvamizi wa Urusi, ambao maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema umewalaazimisha watu zaidi ya milioni 1.7 kuikimbia nchi hiyo.
Hii leo rais Zelenskiy atawahutubia wabunge wa Uingereza kupitia vidio, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais wa taifa jengine kuhutubia bunge hilo kuu la Westminster.
Zelenskiy ambaye amezungumza mara kadhaa na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson tangu uvamizi wa Urusi, ametoa hotuba kadhaa zilizovutia hisia kwa viongozi wa magharibi katika wiki iliyopita, akiwaomba vifaa na msaada wa kijeshi.
Kwa msaada wa DW
Post a Comment