MAFANIKIO YA WIZARA YA KILIMO NDANI YA MWAKA MMOJA UONGOZI WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN.
Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe akizungumza na waandishi wa habari
wakati akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ndani
ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan.
.........
Wizara
ya Kilimo imesaini Hati ya Makubaliano ya miaka mitano na Kampuni ya Smart
Import and Export ya Misri kwa ajili ya ununuzi wa mahindi ya njano na Rasimu
ya makubaliano ya kuiuzia India mazao ya jamii ya mikunde hususan mbaazi
imeandaliwa na taratibu zinaendelea.
Amesema hayo leo Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein
Bashe wakati akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja
ndani ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Amesema Serikali imeongeza bajeti ya utafiti
kutoka Sh. Bilioni 7.35 hadi Sh. Bilioni 11.63, huduma za ugani kutoka Sh.
Milioni 603 hadi Sh. Bilioni 11.5, umwagiliaji Sh. Bilioni 17.7 hadi Sh.
Bilioni 51.48, uzalishaji wa mbegu kutoka Sh. Bilioni 5.42 hadi Sh. Bilioni
10.58.
Aidha amesema Serikali imezipatia NFRA na CPB
jumla ya Sh. Bilioni 129 kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka ambayo
yatauzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Sanjali na hayo Waziri Bashe amesema Wizara
imefanikiwa kufungua masoko mapya ya mazao nje ya nchi ikiwemo soko la
parachichi (India na Afrika Kusini) na ndizi (Kenya) baada ya kukidhi viwango
vya ubora.
“Kumekuwa na changamoto za Utafiti pamoja na
soko la uhakika la mazao, mkulima akiwa hana uhakika wa soko inamlazimu kuacha
kilimo, Serikali imeangalia ni namna gani tunaweza kutengeneza masoko kwaajili
ya kuuza mazao yetu “.Amesema Waziri Bashe.
Waziri Bashe amesema CPB imefungua vituo vya
mauzo katika miji ya Juba (Sudan Kusini) na Lubumbashi (DR Congo) na kukodi
maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 na 2,000 mtawalia.
Ameeleza kuwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.63
zimetolewa kwa ajili ya kuwezesha TARI, TORITA, TRIT, TPHPA na TACRI kuwezesha
utafiti wa mazao ya kilimo ikiwemo mchikichi, zabibu, mkonge, ngano, alizeti, kahawa,
chai na tumbaku.
Amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Wizara ni
pamoja na kuongeza ukuaji wa Sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 za sasa
kufikia asilimia 10, kuongeza mchango wa Sekta kilimo kwenye GDP kutoka 25%
kufikia 35% ifikapo 2030 na kupunguza umaskini kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka
asilimia 26.4 za sasa kufikia asilimia 13 ifikapo 2030.
Post a Comment