Ads

WATAFITI WAIPIGIA CHAPUO SEKTA ISIYO RASMI.

Nchi yoyote Duniani ili iweze kuendelea na kutatua changamoto zinazoikabili, utafiti hauepukiki na umetoa suluhu nyingi katika kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa.

Katika muendelezo uleule Vyuo vikuu nchini vinafanya tafiti kila iitwapo leo na matokeo ya tafiti hizo zimelisaidia Taifa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali nchini.

Hivi karibuni Chuo Kikuu cha Mzumbe kwakushirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi na Roskilde cha nchini Denmark kikiangazia zaidi na kupaza sauti yake juu ya sekta isiyo rasmi na kutoa mapendekezo kwa serikali na wadau ili kuisaidia sekta hiyo ambayo ni mhimili wa uchumi nchini.

Vyuo hivyo vitatu vimefanya utafiti wa aina moja katika mataifa yao na kuziibua changamoto zinazoikumba sekta binafsi na kutoa mapendekezo ili kuzipatia suluhu changamoto hizo.

Utafiti huo wa miaka minne uliofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya na Roskilde cha nchini Denmark umependekeza kuwepo kwa sera na taratibu madhubuti zitakazopelekea sekta isiyo rasmi kupitia vyama vyao kufaidika na huduma za hifadhi ya jamii.

Malengo makuu ya utafiti huo yalilenga kufahamu namna wafanyakazi wasio rasmi kwenye sekta za usafiri, ujenzi na wafanya biashara wadogo Kenya na Tanzania wanavyopata huduma rasmi na zisizo rasmi za hifadhi ya jamii, bima za afya, pensheni, fursa za mikopo, mafunzo mbalimbali kama ya afya na usalama na namna vikundi walivyojiundia vinavyosaidia katika juhudi hizo.

Utafiti huo “Sekta Isiyo Rasmi na Hifadhi ya Jamii” ulioanza 2017-2020 ulifadhiliwa na shirika la kimataifa la maendeleo la Denmark (DANIDA) na kufanywa katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Nairobi na Kisumu.   

Akiongea wakati wa warsha ya kuwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni, Mtafiti na Mratibu Mwandamizi katika Utafiti huo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Godbertha Kinyondo, anasema upo umuhimu kwa taasisi za serikali na wadau kujifunza na kushirikiana na vyama vya wafanyakazi wasio rasmi katika kutunga sera za hifadhi za jamii ili waweze kufaidika na huduma muhimu za kijamii.

“Hili likifanyika litaongeza tija katika sekta zao za kazi, wafanyakazi hawa ni kiungo muhimu katika uchumi,” alifafanua.

Dk Godbetha anasema ni muhimu sasa kwa serikali kupitia taasisi zake mbalimbali kujenga uwezo na kushirikisha vyama vya wadau hao katika kutunga sera zinazogusa maisha yao na kupitia upya programu za hifadhi za jamii ili zikidhi mahitaji mapana ya wafanyakazi hao katika sekta isiyo rasmi, hususani ya usafirishaji inayokua kwa kasi Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla. 

“Serikali ipange kuwa na huduma stahiki za hifadhi ya jamii na rahisi inayoendana na hali halisi kwa wafanyakazi wa kada hii katika sekta ya usafirishaji,” alisema Dkt. Kinyondo.

Mtafiti mwingine wa Chuo Kikuu Mzumbe, Aloyce Gervas anasema sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuchangia pato la taifa kwa asilimia 13 bado ina watu wasio na ujuzi rasmi.  Sekta hiyo pia ndio inayoongoza katika kusababisha ajali za kazini kwa asilimia 23.7 kulinganisha na sekta nyingine.

Hivyo basi Dk Godbetha anaona kabisa kuwa upo umuhimu wa kupitia upya sera ya taifa ya sekta ya ujenzi ili kuwatambua vyema mafundi ujenzi wasio na taaluma rasmi na mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF kutoa elimu ya kutosha kwa mafundi nchini juu ya faida za mifuko hiyo.

“Sera ya Afya na Usalama mahali pa kazi irejewe ili kutambua watu wasio rasmi wanaofanya kazi katika maeneo rasmi kama wajenzi,” alisema.

Mtafiti Mwandamizi toka Chuo Kikuu cha Nairobi, Prof. Winnie Mitullah alisema juhudi za kuboresha sekta isiyo rasmi zinahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali na ushirikiano kati ya nchi na nchi ili kufanikiwa.

“Ni muhimu watafiti, maofisa wa serikali, wadau wa maendeleo, wafanyakazi sekta isiyo rasmi kukaa na kuja na suluhisho litakalokuwa endelevu kwa faida ya nchi zetu,” anasema

Mtafiti, Anne Kamau wa Chuo Kikuu Nairobi anasema suala la hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi bado ni changamoto kubwa nchini Kenya.

“Eneo hili linahitaji mjadala mpana utakaohusisha wadau wengi zaidi ili kuhakikisha sekta isiyo rasmi inafaidika na huduma za hifadhi ya jamii kwa kiasi kikubwa,” anasema Anne.

Akichangia, wakati wa mrejesho wa utafiti huo Rehema Hassan Chuma, Meneja, Kitengo kinachoshughulikia sekta isiyo rasmi, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) anawapongeza watafiti kwa juhudi zao zakufanya utafiti huo na kusema tayari shirika hilo linafanya kazi ya kuongeza wigo wa wanachama kupitia sekta isiyo rasmi tangu mwaka 2018.

“Tutaisaidia serikali kuhakikisha kuwa sera ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi inakamilika,” anasema. Hata hivyo anashauri kuwa umefika wakati sasa kwa makundi kama madereva bodaboda, daladala na wajenzi kujirasimisha katika vyama vitakavyotambulika na kufaidika na huduma kama hifadhi za jamii, na mikopo.

Kwa upande wake Gaston Kikuwi, Mwenyekiti wa chama mwamvuli wa vyama vya sekta isiyo rasmi Tanzania (VIBINDO) chenye vyama 741 na wanachama zaidi ya 68,000 nchini anasema mjadala wa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi sekta isiyo rasmi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi.

“Panatakiwa dhamira ya kweli katika kutekeleza mapendekezo ya utafiti huu kwa faida ya nchi yetu,” anasema Kikuwi.   

Awali, akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka; Dkt. Mary Rutenge anasema utafiti huo unaolenga kuboresha maisha ya wananchi katika nchi hizo mbili ni muhimu na kushauri mamlaka husika kufanyia kazi mapendekezo yake.

Kati ya matokeo mengine muhimu ya utafiti huo ni kuchapishwa kwa kitabu kuhusu hifadhi ya jamii na sekta isiyo rasmi Kusini mwa Jangwa la Sahara kikiangazia mifano halisi katika nchi za Tanzania na Kenya.  Uzinduzi wa kitabu hicho ulifanyika katika warsha hiyo.  Pia, utafiti huo umepelekea kupatikana kwa wanazuoni wawili ngazi ya uzamivu Tanzania na Kenya.

Kwa upande wake mwendesha pikipiki mkazi wa Yombo Vituko kwa Ali Mboa anasema wao wapo tayari kujiunga na kila mfumo wowote na hata kuchangia fedha kwa ajili ya akiba yao ya kesho lakini anasema shida inakuja unapohitaji huduma kwa wakati muafaka.

‘’Sisi kujiunga na kitu chochote chenye manufaa hapa kijiweni kwetu si tatizo ni kijiwe cha waendesha pikipiki tunaojielewa na kujitambua na tunalisha familia zetu na kujikimu kupitia kazi hii shida inayokuja wakati tunapohitaji huduma kuipata kwa wakati nikupe mfano kwenye bima tumekata hizo bima sijui NHIF iliyoboreshwa lakini kupata dawa sasa katika hospitali teule ni mtihani kikubwa watoa huduma wawe  makini katika utoaji huduma na wajali wateja wao sisi ndiyo tunao waweka’’anasema

Kwa upande wake Stephen Chadinga anayejishughulisha na masuala ya Ujenzi katika daraja la Tanzanite Dar es Salaam anasema upo umuhimu wakujiunga na mfumo rasmi kwani hawajui kesho yao.

‘’Kwa sasa huwezi ona umuhimu wa hili lakini shida inapokukuta sasa ndiyo utajua umuhimu wakae lakini pia mfano mfuko wa fidia kwa wafanyakazi ukoleze makali katika kukusanya michango yote kwa waajiri mana michango haipelekwi kwa wakati na hata wakati mwingine unapopata ajali kazini gharama za matibabu ni mtihani,, anasema

Jumla ya madereva daladala 250 na waendesha bodaboda 158 walihusishwa katika utafiti huo Tanzania, wakati wajenzo 212 walihusishwa.  Kwa upande wa Kenya, wafanyakazi 200 katika sekta ya usafirishaji walihusishwa katika utafiti huo.

No comments