WANANCHI WASHAURIWA KUTOA TAARIFA CHANGAMOTO YA MIUNDOMBINU YA BARABARA
Mwambawahabari
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ametoa wito kwa watanzania wote
kutoa taarifa katika Mamlaka za Serikali zinazohusika kuhusu maeneo yote
yenye changamoto iwe ni kwenye madaraja au barabara ambazo zimeharibika
kutokana na mvua nyingi za mwaka huu.
Naibu
Waziri Kwandikwa ametoa wito huo mara baada ya kuwasili mkoani Simiyu
katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari zilizotokana na mvua kubwa
zilizonyesha katika kipindi cha mwisho wa mwaka na zile za mwanzo mwa
mwaka huu katika miundombinu ya barabara ambayo imekamilika na ile
inayoendelea kutekelezwa.
"Niwaombe
watanzania wenzangu mjue kuwa Serikali yenu haipendi mpate shida mahali
kwahiyo mkiona sehemu barabara au madaraja yana changamoto toeni
taarifa hizo katika Mamlaka husika na vitashughulikiwa haraka zaidi
iwezekanavyo", amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Aidha,
Naibu Waziri Kwandikwa amekagua mradi wa ujenzi unaoendelea wa barabara
ya Maswa - Bariadi (km 49.7) kwa kiwango cha lami na kuridhishwa na
kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 78.
Naibu
Waziri huyo amesema kuwa hatua hizi za maendeleo za mradi huu unatokana
na kodi za wananchi na kuwapongeza watanzania kwa kuendelea kuunga
mkono Serikali yao kwa kulipa kodi na hivyo kurahisisha maendeleo ya
mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Hii
barabara inagharamiwa na fedha za ndani hivyo niwahakikishie kuwa kodi
zenu ndio matunda ya miundombinu bora na imara, uboreshaji wa afya,
Elimu na mambo mengine mengi ya kimaendeleo", amefafanua Naibu Waziri
Kwandikwa.
Mapema
akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi Albert Kent, ameeleza kuwa mradi
huo mpaka sasa jumla ya kilometa 17.3 zimekamilika kujengwa kwa kiwango
cha lami na magari yameruhusiwa kupita ili kuepusha usumbufu hasa
vipindi hivi vya mvua.
Mhandisi
Kent amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuusimamia mradi huo ambao
unatakiwa ukamilike mwezi Septemba mwaka huu kwa kuzingatia ubora
unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa.
"Mkandarasi
anaendelea vizuri na kazi ya ujenzi yakiwemo madaraja makubwa mawili
(Daraja la Simiyu na Banhya) na mengine madogo madogo pamoja na ujenzi
wa tuta la barabara katika maeneo mbalimbali", amesema Mhandisi Kent.
Naibu
Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Simiyu
unaohudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 923.65 ambapo
kilometa 334.33 ni barabara kuu, kilometa 521.62 barabara za mkoa na
kilometa 67.7 ni za barabara ya Wilaya ya Nkoma - Makao iliyokasimiwa.


Post a Comment