Waziri Mhagama; Serikali imedhamiria kuwezesha Vijana kushiriki kilimo Biashara.

Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista
Mhagama amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwezesha vijana kiuchumi
kupitia kilimo biashara ili kuchochea ongezeko la ajira na kipato chao.
Ofisi ya Waziri Mkuu
chini ya Baraza la Taifa la Biashara, kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara na Uwekezaji, tayari wilayani Kigoma wameanza kutekeleza Mradi unaolenga
kuwezesha vijana kushiriki katika shughuli za uchumi kupitia mafunzo ya ujuzi na
ujasiriamali kwenye kilimo na ufugaji.
Akiongea katika ziara
yake mkoani Kigoma wakati wa kukagua shughuli za utekelezaji za Baraza la Taifa
la Biashara, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amefafanua kuwa Baraza la Taifa
la Biashara kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na
Uwekezaji, wameanza utekekezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na chuo cha
Maendeleo Kihinga.
“Nitoe wito watendaji
wa Halmashauri na ngazi ya mkoa wa Kigoma waendelee kuwaunga mkono vijana hawa
wanao shiriki katika Mradi huu wa Kilimo Biashara, na nawataka mtambue haya
yote yanafanyika kwa sababu ya jitihada zinazofanywa na Mwenyekiti wa Baraza la
Taifa la Biashara ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli, hivyo ufadhili wa Mradi huu kutoka Mradi wa Kuboresha Mazingira
ya Biashara na Uwekezaji, unaunga jitihada zake za kuwezesha vijana”
Amesisitiza Mhagama.
Naye Mratibu wa Mradi wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Masuala ya Majadiliano ya Sekta
ya Umma na Binafsi), Andrew Mhina alibainisha kuwa katika kuhakikisha unawawezesha
vijana kuwa na ujuzi wa Kilimo na ufugaji utakao wawezesha kujiajiri tayari wameanza
ufadhili wa awali kwa kutoa kiasi cha shilingi
milioni 53 ambazo zimetumika katika Ujenzi wa mabwawa ya samaki,
ukarabati wa mabanda ya kufugia kuku na kuandaa shamba darasa.
Mradi wa Kuwezesha Vijana Kushiriki katika Kilimo
Biashara wilayani
Kigoma, Unaratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara na ufadhiliwa na Mradi wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji chini ya wasimamizi na watekelezaji
wa mradi huo amabao ni; Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Manispaa ya Kigoma, Chuo
cha Maendeleo Kihinga, Chuo cha Uvuvi Kigoma, Maradi wa LIC na Baraza la
Biashara la Wilaya ya Kigoma.
Baraza
la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa
kwenye Gazeti la Serikali Na. 39 la tarehe 28 Septemba 2001. Baraza
la Taifa la Biashara ni jukwaa la majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Lengo kuu la Baraza ni
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa njia ya majadiliano kati ya
sekta ya umma na sekta binafsi. Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Post a Comment