UTUMISHI YAUNGA MKONO KWA VITENDO KAMPENI YA MAKAMU WA RAIS, MHE. SAMIA SULUHU YA KULIFANYA JIJI LA DODOMA KUWA KIJANI KWA KUPANDA MITI
Mwambawahabari
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro akizungumza kuhusu ofisi yake kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya kulifanya
jiji la Dodoma kuwa la kijani iliyozinduliwa
na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya watumishi wa ofisi yake (hawapo
pichani) kukamilisha zoezi la upandaji miti katika ofisi inayojengwa Ihumwa
kwenye mji wa serikali jijini Dodoma.
..................................................................
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeunga mkono kwa vitendo kampeni iliyozinduliwa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya
kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kupanda miti katika ofisi yake
inayojengwa Ihumwa jijini Dodoma kwenye mji wa serikali.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya watumishi wa ofisi
yake kukamilisha zoezi la upandaji wa miti katika mji wa
serikali Ihumwa, eneo ambalo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora inajengwa ili kutoa huduma kwa umma.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, zoezi la upandaji wa miti katika
eneo hilo ni endelevu na kuongeza kuwa, Ofisi yake itahakikisha miti
hiyo inatunzwa kwa kuimwagilia maji ili hatimaye kuwe na mandhari ya
kijani pindi ofisi yake itakapokamilisha ujenzi wa jengo kubwa.
Naye, mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Bi. Menyeaichi Koka ameongeza kuwa, watumishi
wa Ofisi ya Rais - Utumishi wameitikia wito wa Makamu wa Rais, Mhe.
Samia Suluhu Hassan wa kupanda miti ili kulifanya jiji la Dodoma kuwa
kijani na kuishukuru menejimenti ya ofisi kwa kusimamia vema zoezi
hilo ambalo kila mtumishi amelifanya kwa hiyari na kwa moyo mkunjufu.
Bi. Koka ahaidi kuwa, atahakikisha mti alioupanda anauhudumia vizuri
kwa kuumwagilia maji ya kutosha ili uweze kustawi vizuri na kuwa ni
miongoni mwa miti iliyopandwa na kufanikiwa kukua vizuri na hatimaye
kuchangia jiji la Dodoma kuwa kijani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan alizindua kampeni za kulifanya jiji la Dodoma kuwa kijani Julai
21, 2017 kwa kuongoza zoezi la upandaji wa miti ikiwa ni sehemu ya
kuunga mkono kwa vitendo uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makamo Makuu ya Nchi kutoka
Dar es Salaam kuja jijini Dodoma.

Post a Comment