KIKAO CHA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA KUFANYIKA TAREHE 10 NA 11 JANUARI, 2019 ZANZIBAR

Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa inapenda kuwataarifu wajumbe wa Baraza la Vyama
vya Siasa kuwa, tarehe 10 na 11 Januari, 2019 kutakuwa na kikao cha kawaida cha
Baraza la Vyama vya siasa, kitakachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Shirika la Bima Zanzibar uliopo eneo la Madema barabara ya Michenzani mjini
Unguja, Zanzibar.
Awali
kikao hicho ambacho kilitarajiwa kufanyika tarehe 21 na 22 Desemba, 2018
kiliahirishwa
ili kuwezesha Vyama vya
Siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushiriki kikamilifu katika
uchaguzi mdogo wa tarehe 19 Januari, 2019.
Aidha kikao cha Kamati ya Uongozi
kitafanyika tarehe 8 Januari, 2019 kufanya maandalizi
ya kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa. Kwa kuwa wagombea karibu wote wamepita
bila kupingwa, Mkuu wa Sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa ambaye ni
Msajili wa Vyama vya Siasa Mhe. Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Baraza la
Vyama vya Siasa Bw. John Shibuda wameshauriana na kukubaliana kuwa, ni vyema
kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kifanyike mapema, ili kuwezesha Baraza
kuandaa maoni yake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya
Siasa na kuyawasilisha katika Kamati
husika ya Bunge inayooanza shughuli zake tarehe 14 Januari, 2019.
Kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa
kitatanguliwa na Semina kwa wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu
utaratibu wa kutunga Sheria, itakayotolewa na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Semina itafanyika
tarehe 09 Januari, 2019 katika Ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge Zanzibar zilizopo
eneo la Tunguu.
Baadhi
ya ajenda za kikao zitakazojadiliwa ni pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu
Baraza la Vyama vya Siasa, kujadili muswaada wa Sheria mpya ya Vyama vya Siasa
na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza.
Monica
L. Mnanka
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Elimu kwa Umma
Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Post a Comment