Wawekezaji wa Uturuki Wawasili nchini Kuangalia Fursa za Uwekezaji
Balozi wa Tanzania Nchini
Uturuki Profesa Elizabeth Kiondo na Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania
Ali Davuto Glu wameongoza ujio na mapokezi ya Wawekezaji wa makampuni
saba makubwa ya Nchini Uturuki ambao wamewasili nchini kwa ajili ya
kuangalia maeneo ya uwekezaji wa Viwanda ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono
juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayohimiza Sera ya Viwanda kuelekea
uchumi wa kati.
Wawekezaji hao wameonesha
nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwepo viwanda, Kilimo na
Sekta ya umeme, ambapo mikoa ya Dodoma na Simiyu imepewa kipaumbele
na wawekezaji hao ambao wataanza zoezi hilo la ujenzi wa viwanda ifikapo
mwezi Juni mwaka 2019.
Akizungumza katika kikao
cha pamoja cha wawekezaji hao na Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC Balozi
wa Tanzania Nchini Uturuki Profesa Elizabeth Kiondo alisema hatua ya
wawekezaji hao kuonesha nia ya kuwekeza nchini inatokana na mazingira
mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini pamoja na juhudi za kuwahamasisha.
“Ndugu zangu Wawekezaji
hawa wamekuja wakati muafaka kabisa wakati ambao Serikali yetu inahimiza
uchumi wa viwanda,pia ni kwa sababu Serikali yetu imeweka mazingira
mazuri ya uwekezaji,lakini pia tumekuwa tukiwahamasiaha waje kuwekeza
hapa kwetu Tanzania” Alisema Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Profesa
Elizabeth Kiondo.
Alisema bado wana kazi
kubwa ya kuhamasisha wawekezaji wa kutoka Uturuki kuja Tanzania kuwekeza
kwenye sekta mbalimbali na hivyo ujio wao ni mwanzo tu wa wawekezaji
wengine kuja kuangalia fursa na mazingira yaliyopo.
Nae Balozi wa Uturuki
Nchini Tanzania Ali Davuto Glu alisema Tanzania inaelekea kufikia malengo
makubwa ya kiuchumi hali inayoungwa mkono na Serikali ya Uturuki na
kuamua kuwahamasisha wawekezaji wa nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.
“Tanzania inafikia
malengo ya kiuchumi iliyokusudiwa, Sisi Uturuki tunaunga mkono
mambo yote ya kukuza uchumi yanayofanywa na Serikali ya Tanzania, katika
kuhakikisha inapiga hatua za kiuchumi tumeamua kuwahamasisha wawekezaji
hawa waje wawekeze” alisema Balozi Davuto Glu.
Kwa upende wake Mkurugenzi
wa uhamasishaji na Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC John
Mnali alizitaka taasisi zinazohusina na maeneo ya uwekezaji kutoa ushirikiano
kwa wawekezaji hao ili kurahisisha kazi hiyo kufanywa kwa wakati.

Post a Comment