SERIKALI YAHIMIZA JAMII KUTOKOMEZA MILA NA DESTURI KANDAMIZI KWA WANAWAKE
Mwambawahabari
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto) (kushoto)
akiungana na viongozi wa Halmashauri ya Chamwino Mkoani Dodoma katika
kupuliza kipenga cha kuashiria uzinduzi wa awali wa Maadhimisho ya Kitaifa ya
Siku ya Wanawake wa Vijijini kuandaliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini katika
Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.Picha
na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Serikali imehimiza jamii
ya watanzania kutokomeza mila na desturi kandamizi na zenye madhara ili
kuwawezesha wanawake, wasichana pamoja na jamii yote inayoishi vijijini
kunufaika na miundombinu na huduma za kijamii na kiuchumi zinazoendelea
kuboreshwa hapa nchini
Hayo yamesemwa leo
wilayani Chamwino Mkoani Dodoma na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. John JIngu alipokuwa akihutubia wanawake na wasichana
waishio vijijini kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Ally
Mwalimu (Mb.) katika Maadhimisho ya
Siku ya Kimataifa ya Wanamke wanaoishi vijijini iliyofanyika kwa mara ya kwanza
kitaifa mkoani Dodoma katika kijiji cha Manchali B, Kata ya Manchali wilayani
Chamwino.
Dkt.
Jingu amesema kuwa kwa mwaka huu Kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake
Wanaoishi Vijijini inasema ”Kuelekea
Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Miundombinu, Huduma za Jamii kwa Wanawake na
Wasichana Wanaoishi Vijijini” na imezingatia vipaumbele vya kitaifa na muktadha wa nchi
yetu na msisitizo mkubwa amabao umewekwa katika kufikia uchumi wa viwanda na
maendeleo ya watu hususan wanawake na wasichana wanaoishi vijijini kama
ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Taifa wa Pili wa Maendeleo 2015/16
– 2020/21 pamoja na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na
Watoto 2016/17 – 2021/22.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yamewaleta pamoja
wanawake, wanaume, wasichana na wanaume wanaoishi kijijini wakiwemo watunga
Sera, Asasi za Kiraia, wadau wa maendeleo na Taasisi Binafsi kwa lengo la
kutafakari na kujadili kuhusu fursa na changamoto za Mwanamke anayeishi
kijijini.
Dkt. Jingu ameisisitiza jamii kutambua na kuthamini
mchango wa kundi hilo hususan katika kuimarisha uchumi wa viwanda na maendeleo
ya kilimo pamoja na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha hali ya wanawake na
wasichana wanaoishi vijijini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Vumilia Nyamoga amesema kuwa
kupitia maadhimisho haya wanawake wanaoishi kijijini watapata nafasi ya
kufahamu jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali na pia watapata
fursa ya kutoa mrejesho wa namna ya kuboresha afua na huduma hizo.
Kwa upande wake Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) Bi. Hodan Addou ameahidi
kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwasaidia wanawake na wasichana waishio
vijijini kutafakari, kutathmini na kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na
jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo
uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, uboreshaji wa huduma za afya, uboreshaji wa
miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara, uwezeshaji wa upatikanaji wa huduma za
umeme vijijini.
Aidha Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi amesema kuwa wanawake wa kijijini ni
nguzo ya familia na taifa kwa ujumla kwani kwa asilimia kubwa maendeleo ya nchi
yanaletwa na wanawake hasa wanawake waishio vijijini.
Naye mmoja wa wanawake wa kijiji cha Manchali kilichopo
wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Bi. Rose Masima ameiomba Serikali kuwasaidia
wananwake wa kijijini kupata mikopo kutoka mfuko wa wanawake WDF kwani imekua
bado haiwafikii wanawake hao.
Post a Comment