Ads

MKUU WA WILAYA YA TEMEKE ASHIRIKI KUFANYA USAFI NA BENKI YA KCB


          Mkuu wa Wilaya ya Temeke  Mh. Felix Lyaniva akishirikiana na wafanyakazi wa Benki wa KCB pamoja na   wafanyabiashara wa eneo la Mbagara Zakiem wakifanya          usafi katika eneo hilo mapema leo jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mh. Felix Lyaniva ameiomba Benki ya KCB  kutoa huduma nzuri na bora kwa wakazi wa Mbagara, na ikiwezekana kuwapa punguzo la riba na masharti nafuu katika mikopo ili kuweza kupata wateja wengi zaidi.

Ameyasema hayo mapema leo jijini Dar es salaam wakati akifungua zoezi la usafi katika wilaya hiyo lililofanywa na benki ya KCB maeneo ya Mbagara Zakiem, na kuwaomba punguzo hilo kwa kuwa eneno hilo lina wafanyabiashara wengi wadogo na wanahitaji kupewa nguvu ili waweze kufikia malengo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke  Mh. felix Lyaniva akiongea na wafanyabiashara pamoja na wafanyakazi wa KCB benki mapema leo jijini Dar es salaam.

Aliendelea kusema kuwa anafurahia kuona wawekezaji wengi wanaendelea kuwekeza katika wilaya ya Temeke kwani anategemea ubora wa huduma kwa wananchi wake, lakini pia watamsaidia katika shughuli nyingi za kijamii ikiwemo kujenga Madarasa, Zahanati na hata huduma za usafi katika maeneo hayo kwani ndio malengo ya serikali ya awamu ya tano.

Mkuu wa wilaya huyo aliendelea kusisitiza kuwa zoezi la usafi liwe ni endelevu kwani yeye anafanya usafi kila jumaa mosi na sio mpaka iwe jumaa mosi ya mwisho wa mwezi, lakini pia alisema anashukuru kupata wasaidizi kwani alikuwa akipata usumbufu mkubwa hasa katika eneo hilo la Zakiem.
Meneja Masoko wa KCB Benki Christina Manyeye akitoa ufafauzi kwanini leo wameamua kufanya usafi katika eneo la Mbagara. 

Kwa upande wake Meneja Masoko wa KCB Benki Christina Manyeye alisema kuwa wameamua kufanya zoezi hilo ili kuonyesha ushirikiano kati yao na wafanyabiashara pamoja na wakazi wa maeneo hayo, japo kuwa ukiliangalia zoezi hilo kwa haraka haraka utaliona kama ni dogo lakini kwao lina maana kubwa sana.

Aliendelea kusema kuwa KCB Benki inaendelea kuwawezesha wafanya biashara wadogo wadogo katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi, kama leo ilivyotoa zawadi za vitendea kazi kwa wafanyabiashara wa eneo hilo kama miamvuli ya biashara na zawadi nyinginezo.

Na mwisho alipenda kutoa shukrani za dhati wadau waliofanikisha zoezi hilo kwenda mbele wakiwemo, Clouds Media Group, kampuni ya usafi ya West Pro, Creative Company, Pamoja na kampuni ya Proper Media.


No comments