Ads

WAHITIMU VYUO VIKUU KUWEZESHWA

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limebuni mkakati maalumu utakaotoa fedha kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu, watakaoibuka washindi kwa kuandika mapendekezo bora ya kibiashara yanayohusu utalii, kilimo, nishati mbadala na masuala ya mazingira.
Mkakati huo wa NEEC wanaoshirikiana na Ubalozi wa Uholanzi utawalenga zaidi vijana wa umri kati ya 18 na 35, katika kuanzisha na kuendeleza biashara watakazozifanya ambazo siku zijazo zitaweza kuwaajiri vijana wengine ili kupunguza changamoto  ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa amesema jijini Dar es Salaam kuwa, kwa kuanzia, vijana watakaojitokeza wataanza na programu maalumu ya mafunzo itakayowalenga vijana 50 kutoka vyuo vikuu nchini kuwapa ujuzi na kuwawezesha.
“Vijana tutaowachukua ni wale ambao ndiyo kwanza wametoka vyuoni, lakini pia wale ambao walihitimu masomo yao miaka mitano iliyopita pia wanakaribishwa kuhudhuria programu hiyo ambayo itawawezesha wao kuanza na kukuza biashara mbalimbali watakazokuwa nazo,” amesema.
Amesema vijana wanaotaka kuhudhuria programu wanapaswa waandike pendekezo la biashara kwenye maeneo ya utalii, kilimo, nishati mbadala au mazingira.
Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi aliongeza kuwa kwenye mafunzo hayo, programu ya wiki moja ya ujasiriamali itafanyika na itawasaidia vijana kupata mbinu za kijasiriamali ikiwemo kujua jinsi gani ya kuendesha biashara kisha wataandika pendekezo ambalo litashindanishwa kwenye mashindano.
“Vijana ambao watachaguliwa kwa ajili ya kozi ya wiki moja, wataandaa pendekezo kwa ajili ya kushindana na washindi watatu watapewa zawadi. Mshindi wa kwanza atapata Sh milioni 10, wa pili atapewa Sh milioni saba wakati wa tatu atajishindia milioni tano,”amesema.
Aidha, amesema kuwa washiriki wengine watanufaika na mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na ujuzi wa masuala ya biashara.
Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul alisema kuwa programu hiyo itasaidia vijana kwenye masuala ya kuongeza ujuzi kwenye ujasiriamali na hivyo kupunguza tatizo la ajira.

No comments