Mfumuko wa Bei wa Taifa Umepungua Kufikia Asilimia 3.3
Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2018 umepungua
hadi kufikia asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.4 mwezi Juni,
2018.
Hayo yameelezwa leo na Jijini Dodoma na Mkurugenzi
wa sensa na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo
alipokuwa akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai mwaka
huu.
Kwesigabo amesema, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa
na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 imepungua ikilinganishwa
na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018.
"Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia
mwezi Julai, 2018 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa
baadhi ya bidhaa za vyakula, ambapo bidhaa za vyakula zilizochangia
kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai, 2017 na Julai 2018 ni pamoja
na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5, mtama kwa asilimia 17.8, unga wa
mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2,
maharagwe kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5,"
amefafanua Kwesigabo.
Ameendelea kusema kuwa ni zaidi ya miaka 15 tangu
itokee tarakimu kama hiyo ya mfumuko wa bei ambayo iko vizuri kwa uchumi
wa nchi.
Aidha ametaja hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya
nchi za Afrika Mashariki kama ifuatavyo; Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka
ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia
2.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018. Kwa upande wa Kenya mfumuko
wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia
4.35 kutoka asilimia kutoka asilimia 4.28 kwa mwaka ulioishia mwezi
Juni, 2018.
Mfumuko wa bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi
ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi
nchini.
Post a Comment