Ads

MAREKANI YAONYESHA WASIWASI UCHAGUZI MDOGO

Marekani imeonyesha wasiwasi wake kuhusu uchaguzi mdogo uliofanyika  Agosti I2 mwaka huu hapa nchini.

Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam inasema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia na makosa, ikiwemo visa ambapo tume ya uchaguzi nchini humo ilikataa kusajili wagombea wa upinzani.

Ubalozi huo pia ulikuwa na wasiwasi kuhusu vitisho vilivyofanywa na maafisa wa polisi dhidi ya wanachama wa upinzani, kukamatwa kiholela, na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

''Maswala hayo yanahujumu haki ambayo katiba ya Tanzania inawapatia raia wake na kuhatarisha amani na utulivu nchini na katika eneo zima'', ilisema taarifa hiyo.

Agosti I2 mwaka huu hapa nchini kulikuwa na  uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Buyungu, jimbo la Kigoma na kata 36.

Uchaguzi wa Buyungu ulifanyika ili kujaza kiti cha marehemu Kasuku Bilago kutoka chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) aliyefariki mnamo mwezi Mei mwaka huu.

Mgombea wa Chama cha mapinduzi (CCM) Christopher Chiza, ambaye ni waziri wa zamani alitangazwa mshindi wa eneo bunge hilo na tume ya uchaguzi (NEC).

Kulingana na NEC, Chiza alijipatia kura 24,578 na kumshinda mgombea wa Chadema Elia Fredrick Michael aliyejipatia jumla ya kura 7,668. Fredrick alijipatia kura 16,910.

Katika Kata  zote 36 ambapo uchaguzi huo ulifanyika madiwani wa chama cha CCM walitangazwa washindi wa kata hizo.

Viti hivyo vilikuwa wazi baada ya baadhi ya madiwani kujiuzulu kutoka upinzani na kujiunga na chama tawala CCM, vifo mbali na wale waliopoteza uanachama wa vyama vyao kwa sababu zisizojulikana.

CHAMA TAWALA CHA CCM NDIO KIMBILIO LA WAPIZANI.
Kwa takribani mwaka sasa viongozi wa ngazi mbalimbali katika vyama vya upinzani wamehamia CCM.

Kwa zaidi ya wiki moja mfululizo wanasiasa ikiwemo wabunge na madiwani kutoka chama cha CUF na Chadema wametangaza kujiengua katika vyama vyao ikiwemo kujiuzulu nafasi zao za uongozi.

Naibu meya wa manispaa ya ilala, na diwani wa vingunguti Omari kumbilamoto amejiuzulu nafasi ya udiwani na umeya lakini pia amejivua uanachama wa CUF.

Mbunge wa jimbo la Monduli kwa Tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Julius Kalanga Laizer amejiuzulu na kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Magufuli.

Kabla ya kalanga kujiuzulu alikuwa ni mwanasiasa wa upinzani, Mwita Waitara alitangaza kujiengua katika chama kikuu cha upinzani cha chadema na kujiunga na Chama tawala, CCM.

Waitara aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga lililopo Dar es salaam alikishutumu chama cha Chadema, kuwa hakina demokrasia pia kutokuwa na maelewano na mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe.

Ikumbukwe kuwa wabunge hawa wote yaani Waitara na Kalanga waliwahi kuitumikia CCM, ambapo Waitara aliitumikia CCM mwaka 1998 mpaka mwaka 2008 wakati Kalanga aliwahi kuwa diwani kupitia CCM.

No comments