Ads

WATUMISHI WA KIKE MANISPAA YA ILALA WAJITOSA UJENZI VYOO VYA MTOTO WA KIKE.


Mwambawahabari WATUMISHI Wanawake katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wameamua kuanzisha kampeni maalumu ya ujenzi wa Choo cha mtoto wa kike kwa kuanza na shule zote za msingi katika manispaa hiyo.


Hivyo uzinduzi wa kampeni hiyo unatarajiwa kufanyika Oktoba 11 mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema na imani yao ni kwamba wadau mbalimbali wataungana na watumishi hao katika kufanikisha ujenzi wa choo cha mtoto wa kike.
Mratibu wa kampeni hiyo ambaye pia ni Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala Tabu Shaibu amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa watumishi wanawake wa manispaa hiyo wanatambua na kuthamini jitihada kubwa za Serikali na wadau wa maendeleo za kukabiliana na changamoto za mtoto wa kike.

Akitoa sababu za ujenzi wa choo cha mtoto wa kike, Shaibu amesema kila ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka ni siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike duniani na lengo la maashimisho hayo ni kuilimisha na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutetea haki za mtoto wa kike.

"Tafiti zimefanyika kuhusu sababu zinazochangia mahudhurio hafifu ya mtoto wa kike darasani hasa  wa darasa la saba na takwimu zao zinabainisha wasichana wa darasa la saba hawahudhurii shuleni kati ya siku nne hadi tano kila mwezi.Vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia hedhi huleta changamoto kubwa kwao.

"Kutokana na changamoto hiyo watumishi wanawake wa Manispaa ya Ilala wameona wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na kuendelea kuihamasisha jamii na wadau kujenga choo bora cha kisasa kitakachokuwa rafiki kwa mtoto huyu wa kike,"amesema Shaibu.

Mratibu wa Kampeni cha ujenzi cha choo cha Mtoto wa kike ambaye pia ni Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Tabu Shaibu (katikati) akizungumzia maandalizi ya uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo unaotarajia kufanyika Oktoba 11 mwaka huu katika hoteli ya Lamada. Kulia ni Mwenyekiti wa kampeni hiyo na Ofisa Elimu Msingi manispaa ya Ilala Elizabeth Thomas na kushoto ni moja ya wajumbe wa kampeni hiyo.

No comments