Ads

MAMBO MUHIMU YALIYOFANYIKA LIGI KUU ENGLAND

Mohamed Salah alivunja rekodi ya ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya England baada ya kuwafungia Liverpool mabao 38 michuano yote msimu huu. 

Hilo ni moja tu kati ya matukio muhimu yaliyotendeka siku ya mwisho msimu huu wa 2017/18 Ligi ya Premia Jumapili.
Mabao ya Salah yaliwasaidia Liverpool kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Bao la Salah la 32 ligini msimu huu lilimuwezesha kuwapita Alan Shearer, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez. Dejan Lovren alifunga kwa kichwa, Dominic Solanke akafungia Liverpool bao lake la kwanza naye Andrew Robertson akafunga jingine na kukamilisha ushindi wa 4-0 wa klabu hiyo ya Anfield dhidi ya Brighton.
Klabu hiyo ilikuwa inahitaji alama moja pekee kuwapita Chelsea na kujikatia tiketi ya kucheza ligi hiyo kuu ya klabu msimu ujao.
Chelsea, waliopokezwa kichapo cha kushangaza na Newcastle sasa watacheza Europa League baada ya kumaliza nafasi ya tano.
Ushindi wa Liverpool hata hivyo haukutosha kuwafikisha nafasi ya tatu kwenye jedwali ambayo ilitwaliwa na Tottenham waliopata ushindi wa 5-4 dhidi ya Leicester kwenye mechi ambayo huenda ikawa yao ya mwisho kuchezea Wembley kama uwanja wao wa nyumbani kabla ya kuhamia uwanja wao mpya White Hart Lane.
Vijana hao wa Mauricio Pochettino walijipata nyuma mara tatu, lakini Erik Lamela na Harry Kane walifunga mabao mawili kila mmoja, Kane akifikisha magoli 30 ligini, naye Christian Fuchs akajifunga na kuwapa ushindi.
Mwenzake Kane katika timu ya taifa ya England Jamie Vardy alifunga mabao mawili pia siku hiyo lakini upande wa Leicester.
Iwapo Liverpool wangeshindwa na Brighton, bado hawangekosa nafasi ya kumaliza katika nafasi ya nne baada ya Chelsea kulazwa 3-0 ugenini Newcastle.
Ayoze Perez alifunga mabao mawili baada ya Dwight Gayle kufungua ukurasa wa mabao na kuhakikisha Newcastle wakiwa mikononi mwa Rafael Benitez walimaliza nafasi ya 10 kwenye jedwali. Chanzo BBC

No comments