Ads

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) YA TAKA HAKI ITENDEKE KWA WAFUASI WANAOSHIKILIWA POLISI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

Kutokana na Mamlaka za Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala na Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa pamoja kuendelea kuwashikilia watu 25, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinyume cha sheria, Chama kimewaagiza wanasheria wake kuchukua hatua zaidi za kisheria kwa kuwasilisha maombi ya 'Habeas Corpus', Mahakama Kuu, iwapo jeshi hilo halitawaachia au kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao kama taratibu zinavyotaka.

Chama kimeagiza hatua hiyo baada ya jeshi hilo kuonekana kuendeleza utaratibu unaovunja haki na sheria kwa kuwakamata watu na kuwashikilia mahabusu za Polisi kinyume na matakwa ya taratibu za nchi.

Tangu jana asubuhi hadi jioni hii, jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kumshikilia kinyume cha sheria Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, John Heche (Mb) huku kukiwa hakuna dalili za kumwachia au kumfikisha mahakamani ili atendewe haki, ikiwemo kusikilizwa mashtaka yake na kupata dhamana.

Halikadhalika jeshi hilo Mkoa wa Ilala linawashikilia watu 24, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA waliikamatwa jana wakiwa maeneo ya Mahakama ya Kisutu wakifuatilia hatma ya Viongozi Wakuu wa Chama mahakamani hapo.

Katika idadi hiyo ya watu 24, wamo pia watu wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida katika maeneo hayo lakini nao walikumbwa na 'kamatakamata' hiyo ya Jeshi la Polisi iliyofanyika jana maeneo yaliyo jirani na mahakama hiyo.

Aidha, katika kamatakamata hiyo, watuhumiwa wengine walijeruhiwa na hadi sasa haijajulikana majeraha hayo yametokana na nini, hivyo wanahitaji kupata haki ya matibabu ya hali zao za kiafya kwa haraka.

Katika maagizo yake, Chama kimewataka wanasheria kuwasilisha maombi hayo ya 'Habeas Corpus' ifikapo saa nne asubuhi ya Alhamis, Aprili 5, 2018, ambapo muda unaoruhusiwa kwa mujibu wa sheria Jeshi la Polisi kuwashikilia watuhumiwa utakuwa umeisha kwa watuhumiwa hao 25 waliokamatwa jana, ili Mahakama Kuu iliamuru jeshi hilo na mamlaka zingine zinazohusika, kujieleza kwanini zinavunja haki na sheria kwa kuendelea kuwashikilia watu hao bila kuwaachia au kuwafikisha Mahakamani.

Yafuatayo ni majina ya watu hao 25 wanaoshikiliwa na polisi kinyume cha sheria;

1. John Heche (Mb Tarime Vijijini)
2. Lilian Kumei
3.Jonathan Lema
4.Beatrice Mdanya
5.Charles Kakumbi
6.Neema Nyimbo
7.Elizabeth Tossy
8.Ernest Mbuya
9. Damas Mwita
10.Daniel Mshana
11. Paul Shija
12. Jerry  Kerenge
13. Patrick Peter
14. Christina Darabe
15. Adinani Mushi
16. Mbezi Mombeki
17. Jonathan Kimaro
18.  Paulo Makali
19.  Meshak  Mwacha
20. Godfrey Jackson Kayanda
21.  Ramadhani Mkude
22. Happy Baega
23. Novatus  Tesha
24. Jonathan Robert
25. Fikirini Vicent

Tunalaani na kukemea vikali uvunjifu huu wa haki za binadamu na sheria za nchi unaofanywa na Jeshi la Polisi. Tunalikumbusha kuwa kama chombo cha dola kinachohusika na utekelezaji wa sheria za nchi, linatakiwa kuwa mfano ulio bora kwa kutii sheria za badala ya kuzivunja ili kuhakikisha muda wote haki inaonekana ikitendeka katika kutekeleza majukumu yao.

Imetolewa leo Jumatano, Aprili  4, 2018 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments