JK KUSIMAMIA HARAMBEE YA KUCHANGIA SHULE SHILINGI BILION MOJA.
RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alisema harambee hiyo itafanyika Machi 29 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Zambi alisema maandalizi yote kwa ajili ya harambee hiyo yamekamilika na inatarajia kuhudhuriwa na wadau wengine wa sekta ya elimu nchini.
Alisema harambee hiyo imepanga kukusanya Sh. bilioni moja ikiwa ni karibu nusu ya mahitaji ya Sh. bilioni 2. zinazotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kongwe.
“Ni matumaini yetu kuwa kutokana na fedha tutakazokusanya, tumepanga ujenzi uanze wakati wowote. Zoezi hili litakwenda sambamba na mpango wa mkoa kuboresha mfumo mzima wa masuala ya elimu toka ngazi ya awali,” alisema Zambi.
Mkuu wa Mkoa huyo alikiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya inayofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani, akieleza kuwa hatua madhubuti zimechukuliwa ikiwamo kupima uwezo wa walimu.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja changamoto zinazoukabili mkoa huo katika kutoa elimu ikiwamo miundombinu mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo kwa chakula shuleni.
Alisema kuwa ofisi yake imeanza kutekeleza maadhimio ya wadau juu ya namna bora ya kuboresha elimu ndani ya mkoa huo ikiwamo utoaji wa chakula cha mchana mashuleni, mafunzo kwa walimu ili kujenga uwezo wao wa ufundishaji.
Alibainisha kuwa sambamba za zoezi hilo, walimu watakaobanika kuwa na viwango vidodgo vya ufundishaji watashushwa madaraja yao.
Post a Comment