Jukwaa Lamshauri JPM Kuunda Tume ya Kuchunguza Sekta ya Maliasili,Lawataka wanasiasa kutobeza juhudi za na mipango ya Serikali
Mwenyekiti wa Jukwaa la wazalendo Masiga Gulatone , aliyekatikati akizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani aliyepo upande wa kulia ni naibu katibu mkuu Mwanaid Mkina
, na upande wa kushoto ni Mwenyekiti msaidizi Jafari K. Mghamba (Picha na John Luhende)
Mwambawahabari
Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania (JUHWATA) limemshauri Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuunda Tume ya kuchunguza sekta ya maliasili ikiwemo wanyamapori,misitu na utalii inavyonufaisha Taifa.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa JUHWATA, Masiga Gulatone alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu juhudi za Rais Magufuli katika kulinda rasilimali za Taifa.
Ikumbukwe kuwa miaka kadha iliyopita, Tanzania imeshuhudia utoroshwaji wa wanyama wakiwa hai na kupelekwa nje ya nchi, pia tembo wameuawa na pembe zao kusafirishwa isivyo halali na wezi wachache nje ya nchi, hivyo kuathiri sekta ya utalii.
“Nchi yetu imejaliwa na Mwenyezi Mungu utajiri mkubwa wa rasilimali madini ya aina mbalimbali lakini ni ukweli utajiri huu umekuwa ukiwanufaisha watu wachache wasiowaadilifu pamoja na wanaojiita wawekezaji kumbe ni waporaji, wezi na wabadhirifu, huku nchi yetu ikibaki maskini,” alisema Masiga.
Masiga ameongeza kuwa amepatikana shujaa, msomi, mzalendo na jasiri, mpenda haki, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amejitoa kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kusema wizi wa rasilimali za Taifa sasa basi.
Aidha, Masiga amesema kuwa katika kipindi kifupi Rais Magufuli amechukua hatua za msingi katika kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha watanzania walio wengi kwa kuunda Tume mbili zilizochunguza uchimbaji, usafirishaji, uuzaji na kodi itokanayo na madini. Tume hizo ziliongozwa na maprofesa Abdulkarim Mruma na Nehemia Osoro.
“Ripoti hizi zimetupa matokeo chanya kama vile kutungwa kwa Sheria ya Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017, pamoja na marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kuundwa kwa timu ya maridhiano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya madini ya Barrick,”aliongeza Masiga.
Kwa upande wake, Makamu wa Mwenyekiti wa JUHWATA, Japhari Mghamba amewaomba watanzania kuwapuuza watu wanaobeza juhudi za Mhe. Rais katika kulinda rasilimali za Taifa kwani wanasiasa hao hao ndio waliokuwa wakipongeza juhudi za Serikali za kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo kujenga barabara kwa fedha za ndani, sasa wanageuka na kupinga matumizi ya fedha hizo kwa miradi nishati.
“Tunampongeza Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai katika kusimamia maslahi ya Taifa ndani ya Bunge kwa kuunda kamati ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kutimiza azma ya Mhe. Rais Magufuli ya kuhakikisha watanzania tunanufaika na rasilimali hizo,” alisema Mghamba.
Kamati zilizoundwa na Spika ni pamoja na Kamati ya kuchunguza madini ya Tanzanite na ile ya kuchunguza Almasi ambazo zilibainisha upotevu wa madini na ukwepaji wa kodi bila kuinufaisha Tanzania.
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria na inatekeleza kwa vitendo ikiwemo kukomesha wizi, ubadhirifu na vitendo vingine vya kifisadi nchini. Matokeo ya Tume hizo na maridhiano kati ya Tanzania na Kampuni ya Barrick yamekuwa chanya na kuleta tumaini kwa Tanzania kunufaika na rasilimali za Taifa.

Post a Comment