Waziri Mkuchika : Nitaanza na Rushwa, Uzembe Katika Ofisi za Umma
Mwambawahabari
Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menenjimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye sasa amekuwa Waziri wa Madini Angelah Kairuki (kushoto) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora George Mkuchika wakiwa katika hafla ya makabidhiano ya ofisi leo jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni watumishi wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, akizungumza jambo mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katika hafla ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Angellah Kairuki ambaye sasa amekuwa Waziri wa Madini
Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menenjimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye sasa amekuwa Waziri wa Madini Angelah Kairuki akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari katika hafla ya kumkabidhi ofisi mrithi wake Waziri George Mkuchika leo Jijini Dar es Salaam .
Aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angelah Kairuki akimkabidhi nyaraka za ofisi Waziri aliyeteuliwa kuongoza Wizara hiyo George Mkuchika katika hafla iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angelah Kairuki akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari katika hafla ya makabidhiano ya ofisi na waziri aliyeteuliwa kuongoza wizara hiyo George Mkuchika leo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Thobias Robert – MAELEZO
…………
Na: Thobias Robert- MAELEZO
11-10-2017
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kuwa atashughulikia suala la rushwa pamoja na udanganyifu wa umri unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma hapa nchini.
Mkuchika aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam katika mkabidhiano ya Ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo ambaye kwa sasa ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki katika ukumbi wa wizara hiyo.
“Tutaongeza kasi ya kurejesha nidhamu, maadili na mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini,” alifafanua waziri Mkuchika
Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Laurean Ndumbaro pamoja na watumishi wa wizara hiyo, Waziri Mkuchika alisema kuwa atahakikisha anashughulikia suala la watumishi kupandishwa madaraja pamoja na kuongezewa mishahara baada ya kukamilika zoezi la ukaguzi la watumishi hewa.
Aidha alisema kuwa suala la rushwa linatakiwa kujengewa msingi kutoka ngazi ya chini, hivyo ataongea na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ili kuweka somo la rushwa katika mitaala ya elimu hapa nchini kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu.
“Ukienda katika nchi ambazo zimefanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa, mfano Norway, Sweden, pamoja na mataifa ya Scandinavia utakuta wamefanikiwa kwasababu wananchi wote wamepewa elimu dhidi ya rushwa na wanafahamu kwamba rushwa ni adui wa haki, lakini tujiulize watanzania wangapi wanajua kuwa rushwa ni adui wa haki, ni wachache tu,” alisema Waziri Mkuchika.
Aliongeza kuwa, makongamano, semina pamoja na mikutano inayofanya na watumishi wa umma kwa wananchi inapaswa ishirikishe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) ili kutoa elimu juu ya rushwa na kujenga uelewa kwa wananchi kwani itasaidia sana kumaliza tatizo la rushwa hapa nchini.
Waziri Mkuchika alimpongeza mtangulizi wake na kuahidi kuendeleza jitihada alizokuwa akiendelea nazo ikiwemo kuondoa watumishi hewa, vyeti feki, wanaoghushi umri pamoja na uzembe wa wafanyakazi katika ofisi za umma hususani katika Halmashauri.
Kwa upande wake Waziri Kairuki, aliwapongeza watumishi wa Idara, Wakala wa Serikali, Taasisi pamoja na Wizara hiyo kwa ujumla kwa ushirikiano na ushauri walioutoa kwa muda aliofanya nao kazi takribani miaka miwili kwa kuimarisha nidhamu, maadili na kuondoa watumishi hewa katika ofisi za umma.
“Tumeweza kurejesha kwa kiasi kikubwa nidhamu katika utumishi wa umma, tumeweza kwa kiasi kikubwa kuanza kujenga misingi ya kuelekea katika kuboresha masilahi ya watumishi umma maana ilikuwa ni lazima tuanze kusafisha kwanza lakini pia tumeweza kuondoa watumishi hewa, pamoja na kuondoa watu ambao hawakuwa na sifa stahiki katika utumishi wa umma,” alifafanua Waziri Kairuki.
Waziri Mkuchika aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika baraza la mawaziri na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ambapo aliyekuwa anaongoza wizara hiyo Angelah Kairuki aliteuliwa kuwa waziri wa madini.
Post a Comment