Watanzania Watakiwa Kufuata Sheria na Taratibu Za Ujenzi kuepuka Bomoabomoa
Mwambawahabari
Mwakilishi wa makamu mkuu wa chuo cha ushirika moshi Dkt.Lucas Mataba kulia akitoa salam kwa Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya makazi Mhe. Angelina Mabula wa kushoto katika maadhimisho ya makazi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano karimjee Jijini Dar es Salaam leo wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa mipangomiji profesa John Lupala.
mkurugenzi wa mipangomiji profesa John Lupala kushoto akitoa maelezo kwa wadau wa nyumba na makazi katika maadhimisho ya 32 ya makazi duniania yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam kutoka kulia ni Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya makazi Mhe. Angelina Mabula na wa pili kushoto ni Mwakilishi wa makamu mkuu wa chuo cha ushirika moshi Dkt.Lucas Mataba.
Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya makazi Mhe. Angelina Mabula akihutubia katika hafla ya maadhimisho ya 32 ya makazi duniani kutoka kulia ni mkurugenzi wa nyumba Bw.Pius Tesha na wa pili kulia ni mkurugenzi wa mipangomiji profesa John Lupala maadhimisho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi msaidizi wa urasimishaji makazi Bi.Beritha Mlonda akiwasilisha makala ya urasimishaji makazi katika maeneo yaliyoko kwenye mkakati wa mpango wa makazi bora kwa Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya makazi Mhe. Angelina Mabula katika maadhimisho ya 32 ya makazi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano karimjee Jijini Dar es Salaam hivi leo.
Wadau wa nyumba na makazi wakifuatilia mkutano wa maadhimisho ya 32 ya makazi yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano karimjee Jijini Dar es Salaam leo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “sera za nyumba ,nyumba za gharama nafuu”.
Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya makazi Mhe. Angelina Mabula, kulia ni mkurugenzi wa mipangomiji profesa John Lupala na kushoto ni Mwakilishi wa makamu mkuu wa chuo cha ushirika moshi Dkt.Lucas Mataba wakiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa nyumba na makazi wa bodi ya mwenge Jijini Dar es Salaam katika madhimisho ya 32 ya makazi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano karimjee Jijini Dar es Salaam leo.
(picha na paschal dotto- MAELEZO).
………………
Na.Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewataka wananchi kuzingatia Sheria wakati wa ujenzi wa makazi yao ili kuepuka kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa jambo linalosababisha bomoa bomoa isiyo ya lazima.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Angelina Mabula aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Siku ya Makazi duniani ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Karimjee.
Mhe.Mabula alisema kuwa ni vyema wananchi wazingatie sheria kabla hawajaanza kujenga makazi yao husika kwa kutoa taarifa kwenye ofisi husika ili kuepuka ukiukwaji wa Sheria za nchi katika ujenzi wa makazi.
“Watanzania tunakumbushwa kuzingatia Sheria na taratibu za nchi kwa sababu ubomoaji unaofanyika siyo kwa makusudi bali ni kwasababu tu watu wamekiuka Sheria zilizopo na pengine watumishi wasio waaminifu ndani ya Serikali ambao wanawapa watu maeneo pasiporuhusiwa”, alisisitiza Mhe. Mabula
Akizungumuzia mpango mkakati wa Wizara hiyo Mhe. Mabula alisema kuwa zaidi ya Miji 26 nchini ikiwemo Mtwara, Singida Mwanza na Dar es Salaam iko kwenye mchakato wa kupangilia makazi yake na kuwawezesha wananchi kuondokana na adha ya msongamano wa makazi.
Aidha Mhe. Mabula alisema kuwa katika maadhimisho hayo ya 32 yenye kauli mbiu isemayo ‘Sera za Nyumba :Nyumba za Gharama Nafuu’ ambayo inalenga zaidi kuimarisha sera za nyumba na makazi kwa kufuata sheria na taratibu kwa ujenzi wa makazi ya jamii yenye ubora zaidi.
Mhe.Mabula aliongeza kuwa kwa Sera hii ina madhumuni makubwa katika kuhakikisha nyumba na makazi bora yenye huduma za msingi kwa jamii toshelezi ,kuwa na mazingira salama ya kuishi kwa wananchi wote hususani wenye mahitaji maalum wakiwemo watoto, vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu pamoja na upatikanaji wa usafiri na nishati endelevu zenye gharama nafuu ,ili kuwezesha yote haya ni lazima kujua Sheria inasemaje katika kupangilia miji iliyosalama kwa manufaa ya wote.
Alibainisha kuwa huduma nyingine ambazo zinapatikana kwenye makazi yaliyo katika mpangilio mzuri ni upatikanaji wa maji safi na salama na mfumo mzuri wa uondoshaji maji taka kwa ajili ya afya ya binadamu pamoja na uwepo wa hewa safi na ya kutosha.
“Ukienda kwenye eneo ambalo haliruhusiwi kujengwa lazima wakati ukifika kwa wenyewe kulitumia watakuondoa tu kwa sababu si eneo sahihi la makazi kwa hiyo mimi niseme ili kuepuka hii bomoabomoa tusijenge bila kuwa na kibali maalumu kutoka kwenye taasisi inayohusika ili kuweza kukidhi matakwa ya sheria na taratibu za makazi salama”,alisema Mhe. Mabula.
Chimbuko rasmi la maadhimosho ya siku ya makazi duniani lilitokana na Azamio namba 40/202 la baraza kuu la umoja wa mataifa lililopitishwa Desemba,1985 na kuanza rasmi mwaka 1986.
Post a Comment