Baraza la Mji Chake Chake Pemba lazungumza na wafanyabiashara Mwambawahabari
Na Masanja Mabula –Pemba
BARAZA la Mji Chake Chake Pemba limesema mabadiliko ya kanuni katika sheria namba 7 ya mwaka 2014 sheria ya mamlaka ya serikali za mitaa yamelenga katika kuleta ufanisi wa uwajibikaji kwa wafanyabiashara na wananchi wote
Akizungumza na wafanyabiashara hao afisa afya kutoka baraza la mji khamis Abas Machano kwa niaba ya mkurugenzi wa baraza hilo amewataka wafanyabiashara hao kutambua kuwa baadhi ya kanuni za kisheria zimebadilika.
Amesema baadhi ya kaununi hizo zimo zinzowagusa moja kwa moja wafanyabiashara hao, hivyo ndio wakaona kuna umuhimu wa kuwaita na kuwaeleza kwakuwa wafanyabiashara hao ni miongoni mwa wadau wakuu wa baraza hilo
Akitaja kanuni iliyobadilika na inayowahusu wafanyabiashara hao amesema kuwa, kuanzia sasa ada ya usafi imebadilika na kuwa shilingi 1000 badala ya ile ya mwanzo waliyokuwa wakichangia shilingi 600 kwa siku.
Machano amewataka wafanyabiashara kuyapokea mabadiliko hayo kwa mikono miwili kwani hayana lengo baya bali ni kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla huku akisisitiza suala la usafi katika maeneo yao ya kazi .
Aidha amesisitiza kuwa suala la upimwaji wa afya litafanyika kila baada ya miezi sita (6) ambapo kila mfanyabiashara anaeuza chakula anatakiwa kupima afya yake.
“Kila mfanyabiashara anatakiwa ahakikishe anaimarisha usafi katika sehemu yake ya biashara pamoja na kuwa na chombo maalum chenye ufuniko cha kuwekea taka, baraza halitosita kumchukulia hatua mfanyabiashara ambae hatokubaliana na masharti hayo, baraza limejipanga” alisema Machano.
Kwa Upande wake mhasibu wa Baraza la hilo , Khamis Ali amewasisitiza wafanyabiashara hao kutokwenda kinyume na sheria zilizowekwa kwani lengo ni maendeleo kwa wote .
Amefahamisha kuwa kile kinachokusanywa na Baraza hutumika kwa kukirudisha kwa wanajamii wenyewe katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa na baraza hilo kama vile ujenzi wa vyoo katika maeneo yenyeshida hiyo, ujengaji wa madarasa ya wanafunzi katika skuli na mengineyo.
Mpaka kikao hicho kinamalizika , wafanyabiashara hao walionekana kuyapokea mabadiliko hayo kwa lengo la kwenda kuyatekeleza kama sheria zinavyowataka.
Post a Comment