TAARIFA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: TAREHE 16/6/2017
Mwambawahabari
Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inautaarifu umma kuwa Tanzania
inaungana na Nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa
Afrika, tarehe 16 Juni 2017.
Chimbuko la
Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru
za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa
kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa
tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Watoto hao walikuwa
wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za
kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya
elimu ya kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa
tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kupitia Maadhimisho
haya, Serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa
mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi,
walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto
zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, maadhimisho
haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu
maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni
pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi
mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa
ujumla.
Kwa mwaka huu Maadhimisho
haya yatafanyika kimkoa hivyo kila Mkoa utaadhimisha siku hii
kwa kuzingatia mazingira ya mkoa husika.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni
“Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa
Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau
wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na
maendeleo ya Mtoto ilii awezekudhibiti changamoto ya ongezeko la
vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto
wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Wizara inatoa wito kwa
wanahabari, Asasi za Kiraia na wadau wengine kushirikiana na Serikali
katika kuadhimisha Siku hii na kuelimisha jamii kutekeleza kaulimbiu ya
mwaka huu. Utekelezaji wa Kaulimbiu hii utasaidia kuimarisha ulinzi,
usalama wa Mtoto na kutoa haki sawa kwa watoto wote kwa lengo la kufikia
Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.
Mwisho, tunapenda
kuwakumbusha Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja wetu ana
wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanapata Haki zao za Msingi kuanzia
katika ngazi ya familia ambayo ni kitovu cha maendeleo ya Mtoto, jamii
na taifa kwa ujumla.
- Nkinga
KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO – 10/6/2017
Post a Comment