MAREKANI YAAHIDI KUWAJENGEA UWEZO WANAWAKE NA VIJANA WA ZANZIBAR.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala ” Mabodi” akizungumza na Mkurugenzi wa taasisi ya kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia duniani (NDI), Dkt. Keith Jenningspamoja na ujumbe wake
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Sadala amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia Duniani (NDI), kanda ya mashariki na kusini mwa afrika, Dkt. Keith Jennings, huko Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba CCM imekuwa mdau mkubwa wa kutekeleza dhana ya demokrasia kwa vitendo, sambamba na kutoa fursa za uongozi kwa makundi yote ya kijamii.
Alisema ujio wa taasisi hiyo Zanzibar utafungua fursa mbali mbali kwa vijana na wanawake kupata ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kisiasa na kiuchumi.
Pia Dkt. Mabodi aliishauri Taasisi hiyo kufungua Ofisi hapa nchini kwa lengo la kuratibu masuala mbali mbali yakiwemo kuwapatia Vijana fursa za kimasomo nchini marekani ili waweze kujifunza na kupata ujuzi wa fani zinazokubalika katika soko la ajira hapa nchini.
“Vijana na Wanawake wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa ajira, hivyo taasisi yenu ikitoa fursa za mafunzo ya ujasiria mali itasaidia kukabili tatizo hilo.”, alisema Dkt. Mabodi.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya kimarekani inayoshughulikia masuala ya Demokrasia duniani (NDI), kanda ya mashariki na kusini mwa afrika, Dkt. Keith Jennings alieleza kuwa taasisi hiyo inajishughulisha na masuala ya Demokrasia na kutoa mafunzo ya ujasiria mali kwa vijana na wanawake duniani.
Dkt. Keith alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni taasisi hiyo kujitambulisha kwa CCM Zanzibar na kubadilishana mawazo yatakayosaidia kufanya kazi za kisiasa kwa pamoja.
” Taasisi yetu imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mbinu za kutumia fursa zinazopatikana katika mifumo ya Kidemokrasia kwa vijana na wanawake, hivyo tunatarajia hata kwa Zanzibar makundi hayo yatanufaika na mpango huo.”, alieleza Dkt. Keith.
Dkt. Keith alisema Zanzibar ina historia kubwa ya kisiasa hivyo taasisi hiyo ina dhamira ya kuwajengea uwezo vijana mbali mbali hapa nchini ili waweze kutumia vizuri fursa zilizopo katika michakato ya kidemokrasia.
Post a Comment