NGASSA ATAMBA KUIFUNGA SIMBA LEO
Mwambawahabari
Kiungo mshambuliaji mwenye makeke wa Mbeya
City, Mrisho Ngassa, amejiapiza kuwa kamwe hawatakubali kufanywa daraja
la kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara Klabu ya Simba.
Mbeya City na Simba, zinakutana leo Jumamosi kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar katika mechi ya ligi kuu huku Simba ikiwa na
kumbukumbu ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo uliopita.
Katika mechi iliyopita kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, mabao ya Simba yalifungwa na Mohamed Ibrahim ‘Mo’ na Ibrahim Ajibu.
Ngassa alisema kwa maandalizi waliyoyafanya chini ya Kocha Kinnah Phiri, anaamini yanatosha kuwapa ushindi kwenye mchezo huo.
Ngassa alisema, hawataki kupoteza mchezo dhidi ya Simba kwa
lengo la kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo baada ya kupoteza 'Mbeya
Derby' na Tanzania Prisons waliovaana nao katika Kombe la FA ambao
walitolewa kwa mikwaju ya penalti.
“Sitaki kutoa ahadi ya mabao tutakayoshinda na badala yake
mimi binafsi nitaipambania timu yangu kuhakikisha tunaibuka na ushindi
ili tumalize ligi kuu tukiwa katika nafasi nzuri.
"Simba ni timu ya kawaida kama zilivyokuwa timu nyingine na
kwa bahati nzuri timu hiyo niliwahi kuichezea, hivyo ninawafahamu nusu
ya wachezaji niliokuwa nacheza nao pamoja,” alisema Ngassa.
Post a Comment