Mfuko wa Pensheni wa LAPF umekusanya shilingi zaidi ya bilioni 281 katika kipindi cha mwaka 2015/2016
mwambawahabari
PIX 1.Meneja Mafao wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF Bw. Ramadhani Mkeyenge akiwaeleza waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam (hawapo pichani) kuhusu utendaji wa mfuko huo kwa kipindi cha mwaka 2015/2016. Kushoto ni Afisa Masoko Mwandamizi Bi. Rehema Mkamba.
Afisa Matekelezo Mwandamizi kutoka Mfuko wa Pensheni wa LAPF Bw. Kafiti Kafiti (kulia) akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu fursa wanazopata wanachama waliojiunga na mfuko huo. Alioambatana nao pichani ni Maafisa Waandamizi wa mfuko huo.
(Picha na Fatma Salum- MAELEZO)
Na Frank Mvungi-MAELEZO
Mfuko wa Pensheni wa LAPF umekusanya shilingi zaidi ya bilioni 281 katika kipindi cha mwaka 2015/2016 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya mfuko huo kupanua huduma zake na kuwafikia watanzania wengi hasa wanaoishi pembezoni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam Meneja Mafao wa Mfuko huo Bw. Ramadhani Mkeyenge alisema ni dhamira ya mfuko huo kuwainua wananchi kwa kuwasogezea huduma karibu na maeneo yao.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha tunawawezesha wananchi kiuchumi kwa kufanya kazi kwa uadilifu, ufanisi, ari na ujuzi na tumekuwa tukifanya hivi kwa zaidi ya miaka 70” Alisisitiza Mkeyenge.
Akifafanua Mkeyenge alisema kuwa mafao yanayotolewa na mfuko huo ni pamoja na pensheni ya uzee, pensheni ya warithi, pensheni ya ulemavu, mafao ya uzazi, msaada wa mazishi na mafao ya kujitoa.
Akizungumzia mikakati mingine ya kuwawezesha wananchi, Mkeyenge alisema mfuko huo unatoa mikopo ya elimu, mikopo ya saccos, mikopo ya nyumba na mikopo ya wastaafu.
Katika kusogeza huduma zake karibu na wananchi LAPF imekuwa ikiandikisha wanachama kutoka sekta zote binafsi na Serikalini na inajivunia kuwa na ongezeko la wanachama.
Ongezeko hilo linatokana na fursa waliyonayo wanachama ya kuchagua mfuko wanaotaka na ubora wa huduma na mafao yanayotolewa na LAPF.
Hatua nyingine ni kutanua wigo wa wachangiaji kwa kuwafikia wale ambao wako kwenye ajira binafsi kupitia Mpango wa Akiba ya Hiari wa LAPF.
LAPF ina wanachama zaidi ya 165,000 nchi nzima na imefanikiwa kufungua ofisi mpya kanda ya magharibi katika Mkoa wa Geita ili kusogeza huduma katika mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.
Post a Comment