MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WA MIKOA WAJENGEWA WELEDI KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI
Mwambawahabari
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Jinsia Julius Mbilinyi akifungua Kikao Kazi cha Maafisa wa Maendeleo ya
Jamii wa Mikoa (hawapo pichani) katika cha siku mbili kinachoanza leo
katika Hotel ya Edema Mkoani Morogoro.
Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Jinsia Julius Mbilinyi akiwa katika picha ya pamoja na
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa wanaohudhuria kikao kazi kuhusu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto katika mkutano unaofanyika Hotel ya Edema Mkoani
Morogoro.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi
cha Maafisa Maendelo ya Jamaii wa Mikoa wakifuatilia maelezo ya
wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa taifa wa Kutokomeza
Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto katika Hotel ya Edema, mkoani
Morogoro.
………………….
Na erasto ching’oro- Msemaji: Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto leo imefungua kikao cha siku mbili cha Maafisa
Maendeleo ya Jamii wa Mikoa kwa ajili ya kuwajengea uwezo kuhusu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017-2022).
Akifungua kikao hicho, Mwakilishi wa
Katibu Mkuu Bw. Julius Mbilinyi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Jinsia aliwashukuru Washirika wa Maendeleo katika kuhakikisha kuwa
tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto linatokomezwa hapa nchini.
Aliyataja mashirika haya kuwa ni pamoja na UN-WOMEN, Shirika la Idadi
ya Watu Duniani (UNFPA), na Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Haki na Ustawi wa Watoto (UNICEF).
Mgeni Rasimi Kaimu Mkurugenzi wa Jinsia,
aliwapongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa shughuli mbalimbali ambazo
wamekuwa wakizitekeleza katika maeneo yao ya kazi, juhudi ambazo
zimekuwa na mchango katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na
watoto nchini. Alifafanua kwamba, baada ya mafunzo haya, maafisa hao
wataendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kupunguza ukatili kwa
asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/20122.
Wanawake na watoto wamekuwa wakifanyiwa
ukatili kwa kisingizio cha mila na desturi. Aidha, mfumo dume
umesababisha wanawake kutoshiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu
maendeleo yao, katika ngazi ya kitaifa, katika ngazi ya jamii na hata
katika familia zao. Mara nyingi tumesikia wanawake na watoto wakipigwa,
kubakwa na wakati mwingine kuuwawa na watu wa karibu. Vitendo hivi ni
ukatili wa hali ya juu na vinaleta simanzi na madhara makubwa katika
jamii yetu.
Akiongea na Maafisa Maendeleo wa Mikoa,
Bw. Mbilinyi alieleza kuwa madhara ya vitendo vya ubaguzi, unyanyasaji
na ukatili dhidi ya wanawake na watoto huwaathiri kiafya na kisaikolojia
na kijamii ambapo uthoofisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za
maendeleo na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kuiwezesha nchi yetu kuwa
ya viwanda na uchumi wa kati. Wizara kwa kuzingatia changamoto hizo,
imekuwa ikifanya juhudi za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na
watoto, ikiwemo uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili
dhidi ya Wanawake na Watoto.
Katika kuhakikisha kuwa Mpango Kazi huu
unaeleweka na kutekelezwa ipasavyo Wizara imetoa mafunzo kuhusu Mpango
huu kwa wadau mbalimbali. Mafunzo yaliyotolewa ni mwendelezo wa mafunzo
yaliyotolewa kwa waratibu wa Madawati ya Jinsia kutoka katika Wizara,
Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali kuhusu Mpango kazi huo ili
kuwezesha utekelezaji wake.
Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya Jinsia
amefafanua kuwa, Tafiti mbalimbali ikiwemo Taarifa ya Idadi ya Watu na
Afya ya mwaka 2015-2016 inaonesha kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia
bado vipo. Taarifa hii inaonyesha kuwa wanawake 4 kati ya 10 wamewahi
kukumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa wanawake 2 kati ya 10 walikumbana na ukatili
wa kimwili wakati utafiti huo ukifanyika. Ukatili wa kimwili
unaongezeka kadri umri unavyoongezeka; asilimia 22 ya wanawake wenye
umri wa miaka 15-19 wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili,
ukilinganisha na asilimia 48% ya wanawake wenye umri wa miaka 40-49.
Akitoa nasaha zake Afisa Mendeleo ya Jamii
wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Paul Shayo alieleza kuwa mafunzo haya
yatawajengea umahiri, kuweza kutekeleza Mpango Kazi kwa ufanisi. Mbinu
watakazopata zitakuwa mwongozo wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake
na watoto katika jamii.
Vile vile, amekiri kwamba, uzoefu na weledi
utakaoupata kupitia mafunzo haya utawasaidia wahanga wa vitendo vya
ukatili kupata huduma stahiki kwa kuwaunganisha na watoa huduma katika
maeneo mbalimbali.
Mikoa ambayo itajumuishwa katika awamu ya pili ya mafunzo hayo ni Kagera, Mara, Kigoma na Katavi.
Post a Comment